1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Dunia:leo zamu ya Brazil na Korea kaskazini.

15 Juni 2010

Na je, Ivory Coast itatamba ? mzozo wa vuvuzela wahanikiza.

https://p.dw.com/p/Nr6D
Hadi sasa ni bendera ya Ujerumani inayopepea kileleni katika Kombe la dunia 2010.Picha: AP

KOMBE LA DUNIA LEO ZAMU YA BRAZIL:

Baada ya jana mabingwa wa dunia Itali kuzimwa vishindo vyao na Paraguay na kuondoka suluhu bao 1:1,leo usiku ni zamu ya mabingwa mara 5 wa dunia-Brazil kuanza kampeni yake huko Elis Park Stadium,kuania taji la 6 la dunia.

Kwa mashabiki wa Afrika,macho yatakodolewa tembo wa Ivory Coast wanaoutangulia mpambano huo kati ya Brazil na Korea ya Kaskazini ili kupimana nguvu na Ureno itakayotamba na Cristiano Ronaldo.Swali linaloulizwa na kila mmoja ni je,D-D au Didier Drogba alieumia ataweza kuteremka uwanjani ?

MABINGWA WA DUNIA ITALI:

Paraguay,kutoka Amerika Kusini, iliwatilia jana Itali,mabingwa wa dunia,kitumbua chao mchanga walipowafumania ghafula kwa bao mnamo dakika ya 39 ya mchezo kabla Waazuri kusawazisha na kufanya matokeo kuwa bao 1:1.

Waamerika kusini hao, wamekuja katika kombe la dunia wakiwa wamejiandaa barabara,kwani, walikwishailaza Brazil na hata Argentina wakati wa kinyan'ganyiro cha kanda ya Amerika Kusini, kuania tikiti za kombe hili la Dunia la 2010. Sifa nyingi ,zilikwenda kwa kocha wao Paraguay,muargentina, Gerardo Martini, kwa mbinu zake alizotumia jana. Waparaguay, kwahivyo, wametoa salamu kwa timu nyengine kwa kuwastua mabingwa wa dunia.

HOLLAND :UWANJA MPIRA NA VUVUZELA:

Kabla ya changamoto kati ya Itali na Paraguay, kinyan'ganyiro cha tiketi za kucheza duru ya pili katika kundi E baina ya Holland na Denmark , kilisababisha malalamiko mengi tena tangu kwa washindi na hata walioshindwa:

Yameanzia hali ya uwanja uliochezewa mpambano wa jana,mpira wenyewe uliotengezwa na kampuni la Puma hadi zumari la vuvuzela. Mlinzi wa Holland Mark van Bommel, alidai ushindi wa Holland wa mabao 2:0 dhidi ya Denmark haukusaidiwa na hali ya uwanja.Alisahau lakini , kutaja ulisaidiwa na bao walilotia wadeni wenyewe. Uwanja ulikuwa mgumu kuchezea-aliadai.

Van Bommel, alilalamika pia juu ya mazumari ya vuvuzela na ingawa hakudai yapigwe marufuku,alisema yanazuwia mawasiliano uwanjani.Mwenyeji mmoja wa Afrika Kusini ,akitetea mazumari hayo alisema,

"Nadhani ikiwa Afrika Kusini, ni mwenyeji wa Kombe la Dunia, unapaswa kuheshimu desturi zao na ujiunge nao katika shangwe zao.Kwahivyo, haifai kunun'gunika na jiunge tu na shangwe."

Alaasiri hii,kombe la dunia linaendelea kwa New Zealand kupambana na Slovakia kabla Ivory Coast, kuingia uwanjani katika kundi la kufa kupona kupambana na Ureno.

Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE/DPAE

Uhariri: Othman Miraji