1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la klabu bingwa barani Afrika

18 Septemba 2009

Bayern Munich inaumana na Nüremberg .

https://p.dw.com/p/JkBY
Van Gaal-kocha wa B.MunichPicha: AP

-Katika Kombe la klabu bingwa barani Afrika,mabingwa 2 wa zamani wakutana mjini Lumbubashi:Etoile du saheil ya Tunisia na wenyeji wao TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo wakiania tiketi ya nusu-finali ya kombe hilo.

-Vyama vya riadha barani Afrika vyalalamika mageuzi katika kalenda ya michezo duniani yanayoweza kuwaumiza mabingwa wa Afrika hasa -Kenya na Ethiopia.

Kesho ni zamu ya Berlin-marathon -je, muethiopia Haile Gebr-selassie ataweka rekodi mpya ?

-Macho yanakodolewa Premier-League Ligi ya Uingereza ambako jumapili hii mahasimu 2 wa mtaani Manu na Manchester city wanaumana.

MARATHON:

Kesho ni mbio za kila mwaka za Berlin - marathon ambazo miaka ya karibuni, zimekuwa zikitoa changamoto upande wa wanaume na hata wa wanawake kati ya Ethiopia na Kenya.Rekodi ya dunia ya mkenya Paul Tergat ilikuja kuvunjwa na muethiopia mzee Haile Gebrselassie mjini Berlin. Mwaka jana,Haile alikimbia tena mbio hizo huko Berlin na akaivunja tena rekodi yake na kuiweka chini ya masaa 2 na dakika 4.

Kwavile, mashindano ya marathon ya ubingwa wa dunia-world Athletics championship yalianyika Berlin hapo August, wengi walitazamia kwamba mzee Gebrselassie angekimbia mbio hizo ili atawazwe bingwa wa dunia akichanganya na rekodi ya dunia kutoka mji mmoja wa Berlin.

Kwa msangao wa mashabiki wengi wa riadha, Haile Gebrselassie aliamua kutokimbia mbio za marathon za ubingwa wa dunia na badala yake kukimbia mbio za kesho za Berlin marathon. Nani atampa changamoto kati ya madume wa kenya ?

IAAF NA AFRIKA:

Kenya na Ethiopia ndio mataifa makuu ya riadha barani Afrika:mataifa hayo 2 yanatawala mbio za masafa ya kati kuanzia mita 800 na marefu hadi 10.000 na marathon.Kenya na Ethiopia zilitamba pia katika mashindano ya mwisho ya riadha ya ubingwa wa dunia mjini Berlin.Sasa kuna hofu ya mabingwa wa Afrika kunyimwa medani ya kutamba ulimwenguni licha ya ustadi wao.

Chini ya mpango mpya wa mabadiliko ya kalenda za mashindano ya riadha, mashindano ya ubingwa wa mbio za nyika duniani-world cross -country championship- yatabadilishwa . Baada ya kuwa ya kila mwaka sasa yatafanyika kila baada ya miaka 2.Imeonekana kuwa, wafadhili wa TV wamepoteza hamu ya mashindano hayo kwavile, daima ushindi ama ukienda kwa wakenya au kwa waethiopia-hii ni kwa muujibu alivyosema msenegal-rais wa IAAF-shirikisho la riadha ulimwenguni Lamine Diack.

Diack, alinukuliwa kusema, " mbio za nyika ulimwenguni sio tu zimegeuka mchezo wa waafrika wenyewe kwa wenyewe,bali hata kati ya waafrika mashariki wenyewe kwa wenyewe.Hupati hata wanariadha wa Afrika magharibi kushiriki."-Diack aliliambia gazeti la Kenya la DAILY NATION mwezi uliopita.

Mashindano ya wanaume -senior-ushindi daima unaenda ama kwa Ethiopia au Kenya tena kila mwaka tangu 1981.Upande wa wanawake, ni Ureno tu iliotoroka na ushindi 1994 na hivyo, kuchafua ushindi mfululizo wa wasichana wa Afrika ulioanzia miaka 18 iliopita.

Bingwa wa zamani wa mbio hizo za nyika,mkenya Paul Tergat amesema kwamba, uamuzi wa IAAF si haki. Tergat alishinda mbio za wanaume za nyika duniani -senior -kati ya 1985 na 1989.Finali ya mashindano ya riadha ya dunia yaliofanyika mwishoni mwa wiki iliopita kwa muda wa siku 2 huko Thessaloniki,Ugiriki, nafasi yake itachukuliwa na mfumo mpya wa "Diamond League "yatakayofanyika Asia, ulaya na Marekani.Bara la Afrika halitaandaa mashindano yoyote.

Mwaka ujao, finali zitafanyika mwishoni mwa wiki X2: mara ya kwanza Zurich na ya pili Brussel.Thessaloniki ilijionea ushindi mkuu kwa wanariadha wa Afrika walioshinda kila mchezo .Kati ya waliofaulu kukimbia mita 5000,Tisa walikuwa wakenya na watatu pamoja na mshindi Imane Merga, ni waethiopia. Je, sasa waafrika wanaadhibiwa kwa uhodari wao wa michezo ?

Kombe la dunia la riadha, linalowapambananisha waakilishi wa mabara mbali mbali,limetungwa upya kujumuisha bara la Asia na eneo la Ocenia kuunda timu moja na Amerika kaskazini, ya kati na ya kusini zitaunda timu moja.Afrika na Ulaya ndio mabara pekee yatakayoshindana kwa kujitegemea.Pierre Weiss,Katibu mkuu wa IAAF, amesema mageuzi haya yataleta msisimko katika mashindano ya riadha ulimwenguni.

Dube Jilo,mkurugenzi wa kiufundi wa shirikisho la riadha la Ethiopia, akiungamkono kilio cha mkenya Paul Tergat kuwa mbio za nyika ulimwenguni-"world crosscountry championship - ni mojawapo ya mashindano ya kuvutia duniani", Akasema: anaungana na wenzake katika kuvunjwa moyo na uamuzi uliopitishwa na sio kwa Ethiopia pkee bali kwa Afrika mashariki nzima.

Sura inayoibuka nikuwa Afrika ina nguvu za riadha,haina sauti katika halmashauri zinazopitisha maamuzi za Shirikisho la riadha ulimwenguni-IAAF ambamo msenegal Lamine Diack, bado ni rais wake.

Muandishi : Ramadhan Ali