1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Ulaya uwanjani leo

9 Machi 2010

Bayern Munich na Fiorentina.nani atatamba ?

https://p.dw.com/p/MOCm
Franck Ribery, kulia arudi uwanjani leo.Picha: AP

Kinyan'ganyiro cha Kombe la klabu bingwa barani ulaya-Champions League- kinarudi uwanjani leo usiku(Jumaane) na kesho (Jumatano):

Katika mapambano mawili ya jioni hii, mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani, Bayern Munich, wanaitembelea Fiorentina, huko Florence, Itali , wakijaribu kutetea ushindi wao wa kutatanisha wa mabao 2:1 wiki mbili nyumbani katika uwanja wa Allianz Arena.

Katika mpambano wa pili jioni hii, Arsenal ya Uingereza ina miadi na FC Porto ya Ureno kabla kesho David Beckham,akivaa jazi ya AC Milan ya Itali, kurudi uwanjani Old Traford kwa mpambano wa kufa-kupona na timu yake ya zamani, Manchester United.

Bayern Munich, ambayo imetwaa mara nne Kombe hili la klabu bingwa barani ulaya na inaongoza sasa Bundesliga-Ligi ya Ujerumani- licha ya kutoka sare tu mwishoni mwa wiki na FC Cologne,bao 1-1 ,inawarudisha jioni hii uwanjani mastadi wake wawili wa kiungo walioumia: mdachi Arjen Robben na mfaransa Franck Ribery. Baridi kali na pengine theluji, inatazamiwa kuanguka kwa wingi mjini Florence, lakini mashabiki 42,100 wameahidi kuujaza uwanja wakiwaachia wageni wao kutoka Munich, tiketi 3000 .

Upande wa Fiorentina, leo hauwezi kuwategemea mlinzi Alessandro Gamberini wala Muargentina, stadi wa kiungo, Alberto Santana. Lakini Alberto Gilardino ameitwa kuongeza idadi yake ya mabao 4 aliokwishatia katika kombe hili la Ulaya. Adui yake Muargentina mwenzake, Martin Demichellis, anaeichezea Munich, si fit leo kuteremka uwanjani. Aliumia wiki iliopita pale Argentina, ilipoin'goa meno Ujerumani kwa bao 1:0.

Fiorentina inataka jioni hii kufuta lile bao la madhambi alilotia Miroslav Klose wiki mbili nyuma katika hali ya kuotea na ambalo rifu hakuliona.

Katika mpambano wapili jioni hii, FC Porto ina ndoto nyengine ya kucheza finali ya kombe hili la Ulaya. Lakini Arsenal , imeanza kuja juu, kwani imenyatia hadi pointi sawa na Chelsea katika Premier League-Ligi ya Uingereza. Lakini, Arsenal ililazwa na Porto duru iliopita.

Macho ya mashabiki wa Italy na Uingereza, kesho Jumatano, yatakodolewa mpambano kati ya Manchester United na AC Milan huko Old Traford. Kwa David Beckham wa AC Milan, utakuwa mpambano wa kukata na shoka.

Licha ya pigo iliopata nyumbani Italy, AC Milan ilio nyuma ya rekodi ya Real Madrid ya kombe hili kwa vikombe viwili tu,inajua itahitaji miujiza na uchawi wote wa David Beckham, kutamba Old Traford.Wakati AC Milan imekiona cha mtema kuni duru iliopita ilipozabwa mabao 3:2 na Manu , inaelewa vyema bila ya ushindi huko Uingereza, ni kuaga buriani Kombe la ulaya mwaka huu.

Manu haina hakika kwamba jogoo lao, Wyne Rooney, limepona sawa sawa kuliteremsha uwanjani hapo kesho. Rooney aliumia pale Uingereza ilipowachezesha mabingwa wa Afrika, mafiraouni Misri kindumbwe-ndumbwe uwanjani Wembley walipowakomea mabao 3:1.

Kesho pia Real Madrid, mabingwa mara kadhaa wa Kombe hili, wamepania kucheza robo-finali kwa kuitimua nje O. Lyon ya Ufaransa. Cristiano Ronaldo na wenzake walijionoa makali jumamosi walipoikomea sevilla katika La Liga kwa mabao 3-2. Lyon inadai mramba asali, harambi mara moja na inataka ushindi mwengine kesho.

Mwandishi: Ramadhan Ali/DPAE

Uhariri: Miraji Othma