1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano kuhusu fursa za kibiashara Afrika lafanyika Kigali

Sylvanus Karemera25 Machi 2019

Kongamano la kuchambua fursa za kibiashara barani Afrika lafanyika Kigali Rwanda na kuhudhuriwa na wakurugenzi wakuu wa makampuni mbalimbali pamoja na baadhi ya marais barani Afrika.

https://p.dw.com/p/3FcmQ
Ruanda Kigali Unterzeichnung Afrikanisches Freihandelsabkommen
Picha: Imago/Xinhua/G. Dusabe

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema mikakati yote ya kimaendeleo inayochukuliwa barani Afrika kwa kiasi fulani imeshindwa kufikia lengo lake kutokana na sababu za kisiasa. Rais Kagame alikuwa akizungumza jijini Kigali mwanzoni mwa kikao cha siku mbili kinachowajumuisha wadau wa maendeleo zaidi ya elfu moja na mia tano pamoja na viongozi wa baadhi ya serikali za mataifa ya Afrika.

Ni Kongamano ambalo licha ya mamia kwa mamia ya wakuu wa makampuni ya kiuchumi na kibiashara barani Afrika linahudhuriwa pia na marais Faure Gnasingbe wa Togo,Felix Tshishekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sahle Work Zewde wa Ethoipia.

Ni kongamano ambalo kwa kiasi kikubwa linachambua fursa za kibiashara barani Afrika, changamoto zake na nini sekta binafsi pamoja na serikali za kiafrika zifanye ili kuondoa adha hiyo inayoodhofisha ushirikiano wa kibiashara baina ya Waafrika kwa waafrika.

Phillipe Le Houerou mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa kuhusu fedha IFC amesema  Afrika inahitaji kufanya katika kutekeleza mikakati kutokana na mahitaji yaliyopo.

Gharama za usafiri ni changamoto inayokumba sekta ya biashara Afrika
Gharama za usafiri ni changamoto inayokumba sekta ya biashara AfrikaPicha: Imago/Xinhua/Lyu Tianran

"Afrika inahitaji fursa mpya za ajira zinazofikia milioni moja na laki saba kila mwezi.Ni kwa jinsi gani unatengeneza fursa hizo?Ni kutengeneza sekta binafsi yenye nguvu na yenye ushawishi mkubwa na inayowezeshwa na mazingira huru ya kufanya biashara katika bara zima."

Gharama za usafirishaji nazo ni tatizo hasa miongoni mwa waafrika wenyewe kwa wenyewe kama anavyofahamisha Profesa Carlos Lopes wa chuo kikuu cha Cape Town nchini Afrika Kusini.

Gharama za usafirishaji wa kontena kutoka hapa hadi Mombasa ni kubwa kuliko kutoka Mombasa hadi China na hii haiwezi kuruhusiwa iendelee. Na hayo ndiyo yatasuluhishwa na soko la pamoja la Afrika CFTA ili kurekebisha mambo na kurekebisha mambo kunahitaji mazungumzo.

Hata hivyo mazingira huru yanayotajwa ni kama hayapo miongoni mwa mataifa ya kiafrika kutokana na kwamba kile kinachojadiliwa kwenye majukwaa kama hili sicho kinachofanyika kwa vitendo.Rais Paul Kagame akataja kwamba kuwepo kwa tatizo hilo kunatokana na kuingiza siasa nyingi huku akitoa mfano wa sakata baina ya Rwanda na Uganda.

Wadau wanasema ipo haja ya kuwepo mazingira huru yatakayowezesha biashara inawiri barani Afrika.
Wadau wanasema ipo haja ya kuwepo mazingira huru yatakayowezesha biashara inawiri barani Afrika.Picha: Imago/robertharding

Kwa mfano tuna mamia ya watu kutoka Rwanda wanaokamatwa na kuzuiliwa kwenye sehemu zisizofahamika kule Uganda, hii inapoendelea ni sawa na kuwaambia watu wetu kwamba hawatakiwi kule Uganda, hili ni suala ambalo mimi binafsi nimelizungumzia na utawala wa juu kule Uganda kwa muda wa miaka miwili sasa lakini halipatiwi ufumbuzi,lakini hilo tuliweke kando kidogo kuhusu athari za uchumi, kuna makontena yetu na madini yaliyozuiliwa nchini Uganda wakati yakielekea Mombasa nchini Kenya kwa muda wa miezi mitano. 

Na haya si makontena ya raia wa Rwanda, hapana yalikuwa ni mwekezaji wetu kutoka Ujerumani,kuna mamilioni ya lita za maziwa yaliyokuwa yakisafirishwa kutoka Rwanda kuelekea nchini Kenya kwenye viwanda vya Kenya hayo yalizuiliwa pia kwa miezi hadi yakaharibika!

Na hii pengine ikawa sababu japo bila kutajwa ikaifanya Rwanda kuweka nguvu za ushirikiano wa kibiashara na mataifa ya mbali kama vile Gabon na mengine ya kati na magharibi mwa Afrika.Wiki iliyopita Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zilitia saini ya ushirikiano wa safari za anga ambapo ndege ya Rwanda,Rwandair itaanza safari za moja kwa moja baina ya Kigali na Kinshasa kuanzia April 15.