1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la kimataifa la taasisi za habari lamalizika Bonn

Mohammed Khelef
8 Novemba 2019

Kongamano la kimataifa lililowakutanisha mamia ya wanahabari na asasi mbalimbali kutoka mabara yote duniani kujadili mustakabali na maendeleo ya vyombo vya habari lilimalizika jioni ya Ijumaa (8 Novemba) mjini Bonn.

https://p.dw.com/p/3Si2I
 FoME Symposium 2019

Kongamano hilo lililoandaliwa na DW na kupewa jina la FoME lilijadili kwa kina kuhusu fursa na changamoto zinazovikabili vyombo vya habari duniani na pia mbinu za kupata ufumbuzi.

Baadhi ya mada zilizojadiliwa ni mabadiliko ya kiteknolojia, matumizi ya takwimu, uhuru wa vyombo vya habari, upatikanaji na usambazaji wa habari pamoja na mifumo ya kisiasa na demokrasia ulimwenguni.

Changamoto kuu iliyogubika majadiliano ni kubinywa kwa uhuru wa vyombo vya habari katika nchi mbalimbali hususani barani Afrika, Amerika ya Kusini na Asia ambako kunatajwa kutokuwepo na mazingira rafiki kwa vyombo vya habari. 

"Vyombo vya habari vinagubikwa na mbinyo wa kisiasa, hali mbaya ya kiuchumi, sheria na kanuni zisizo rafiki pamoja na kubinywa kwa uhuru wa waandishi wa habari kuandika habari za kiuchunguzi," alisema Pedro Vaca Colombia, mshiriki kutoka Afrika Kusini.

Kongamano la vyombo na wadau wa habari duniani hufanyika kila mwaka kwa lengo la kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazovikabili vyombo na waandishi wa habari kwa kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia na changamoto cha kisiasa.  

Zaidi ya washiriki 100 walihudhuria kongamano la mwaka huu lililokuwa na kauli mbiu ya "Tufikiri Upya Maendeleo ya Vyombo vya Habari."

- Prosper Kwigize