1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongole Deutsche Welle

23 Januari 2013

Redio yetu Kiswahili, napenda gamba vigambo Nyumbani kila mahali, wa mkuruba na ng'ambo Ina ladha na makali, ni idhaa yenye tambo Kongole kwa Deutsche Welle, hamsini kutimia.

https://p.dw.com/p/17QFH
Die Journalistin Grace Kabogo. Januar, 2013, Bonn
50 Jahre Kisuaheli RedaktionPicha: DW

Myaka hamsini tamima, mnatujuza habari
Kitendeti kuyasema, yalofichwa sirisiri
Mumevuka milima, nyanda pia na bahari

Ulaya na Afrika, mashabiki tumbi zima
Asia pia wafika, sifa zako zinavuma
Lau watilia shaka, nenda ukazuru Barma

Korija nakuvulia, wewe usiye mfano
Na koja nakuvishia, kwa ishara ya maneno
Na tungo nakutungia, kishairi pamwe ngano

Langu ombi wahariri, mdumishe kazi njema
Waandishi mashuhuri, msilale ni mapema
Fichueni hizo siri, mtupashe himahima

Wasalaam mashabiki, inshallah tutaonana
Qahari awabariki, kwa marefu na mapana
Idhaa yetu na ibaki, nyota yake ikifana
Kongole kwa Deutsche Welle, hamsini kutimia

Tanbihi: Shairi la Wasuwa Maxwell (Malenga Chipukizi Mtanashati) wa Nairobi, Kenya kwa ajili ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya DW.

Mhariri: Mohammed Khelef