1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kony aahirisha kutia saini makubaliano ya amani

Dreyer, Maja10 Aprili 2008

Kwa mara nyingine tena, kutiwa saini makubaliano ya amani na kiongozi wa kundi la waasi wa Uganda, LRA, Joseph Kony, kumeahirishwa.

https://p.dw.com/p/Dffb
Joseph Kony, kiongozi wa kundi la waasi wa LRAPicha: AP


Kulingana na mtapanishi mkuu, naibu rais wa Sudan Kusini, Bw. Riek Machar, Kony yuko tayari kutia saini, lakini anataka ufafanuzi kuhusu masuala mawili ya makubaliano haya.


Inaonekana kama wakaazi wa Uganda wanalazimishwa kusubiri siku moja nyingine hadi kupata habari kuhusu tukio la kihistoria lililotarajiwa kutokea leo katika kijiji hiki kilioko Kusini mwa Sudan ambapo tangu asubuhi, wazee, wajumbe wa serikali za Sudan na Uganda na wanajeshi wa LRA walikusanyika kumsubiri Joseph Kony kiongozi wa kundi la waasi wa Lord Resistance Army LRA atie saini makubaliano ya amani na hivyo kuvimaliza vita vilivyoendelea kwa muda wa miaka 22 nchini Uganda.


Naibu rais wa Sudan Kusini, Bw. Riek Machar ambaye ni mpatanishi mkuu kati ya kundi la LRA na serikali ya Uganda, mchana huu aliwaambia waandishi wa habari kwamba saini haitatiwa leo. Alikusanya baadhi ya wazee waende kwa Joseph Kony kumfahamisha kuhusu masuala ambayo Kony alitaka yafafanuliwe zaidi. Pia Bw. Machar mwenyewe anataka kukutana na Kony leo au kesho asubuhi.


Naibu rais Machar alieleza kwamba Joseph Kony alikuwa na mashaka kuhusu utaratibu wa sheria ambazo serikali ya Uganda inataka kuzitumia katika mahakama maalum ambayo itashughulikia mashtaka ya uhalifu wa kivita badala ya mahakama ya uhalifu wa kimataifa ya The Hague, Uholanzi, iliyotoa hati za kuwakamata Kony na manaibu wake.


Mwandishi wa habari Mareike Schomerus ambaye yuko huko msituni mwa Kusini mwa Sudan na anayefuatilia hali huyo anaeleza vile makubaliano ya amani yanavyosema juu ya mashtaka hayo: "Makubaliano ya mwisho yatasema kwamba kutakuwa na mahakama itakayoanzishwa nchini Uganda kwa ajili ya kushughulikia kesi zinazohusu masuala ya kesi na zaidi zile zinazohusu LRA na Serikali. Kitakachotokea baada ya kutia saini ni kwamba Serikali ya Sudan itawasiliana na Baraza la Umoja wa Mataifa ambalo lina uwezo wa kuitaka Mahakama ya Umoja huo isimamishwe hati hiyo na kuchunguza endapo mfumo wa sheria wa ndani wa Uganda ikiwa mahakama hiyo maalumu itawahukumu ipasavyo na kuleta usawa".


Mahakama ya The Hague inawashtaka viongozi hao wa LRA kwa uhalifu mbalimbali za kivita zikiwa pamoja na ubakaji, mauaji na kuwateka nyara watoto waliotumika kama wanajeshi au watumwa. Hata ikiwa Kony atakubali kutia saini makubaliano, waasi walisema hawatakubali kuvuliwa silaha zao hadi mashtaka haya yatakapobatilishwa.


Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, anatarajiwa kutia saini makubaliano hayo Jumanne wiki ijayo mjini Juba, Kusini mwa Sudan. Serikali yake ilisema itaiomba mahakama ya The Hague kubatilisha hati zake iwapo makubaliano ya mwisho yatafikiwa. Hakuna uhakika lakini ikiwa serikali inataka waasi wa LRA wapokonywe silaha zao kwanza.


Mahakama yenyewe imesema haitaki kuzuia amani ikiwa mazungumzo yatafanikiwa kumaliza vita hivyo virefu na vikali ambapo maelfu ya watu waliuawa na watu wasiopungua millioni mbili kupoteza makwao.