1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini ilinunua teknolojia kupitia Berlin

Sylvia Mwehozi
6 Februari 2018

Kituo cha utangazaji cha umma nchini Ujerumani kimeripoti kwamba Korea Kaskazini iliutumia ubalozi wake mjini Berlin ili kujipatia vifaa vya teknolojia ya hali ya juu.

https://p.dw.com/p/2sBMQ
Deutschland nordkoreanische Botschaft in Berlin
Picha: pictur-alliance/AP Photo/M. Schreiber

Shirika la upelelezi wa ndani linaamini kwamba teknolojia hiyo ilitumika katika programu ya makombora na mpango wa nyukilia.

Korea Kaskazini ilinunua vifaa na teknolojia kwa ajili ya programu ya makombora ya masafa marefu kwa kutumia ubalozi wake mjini Berlin, amesema mkuu wa shirika la upelelezi wa ndani la Ujerumani BfV, wakati alipozungumza na shirika la utangazaji la umma NDR katika makala iliyoruka siku ya Jumatatu.

"Tuligundua kwamba shughuli za ugavi zilifanyika pale, kulingana na mtazamo wetu katika programu ya makombora pamoja na mpango wa nyukilia", alisema Hans-Georg Maassen.

Hans-Georg Maassen Präsident Bundesamt für Verfassungsschutz
Mkuu wa shirika la upelelezi la BfV, Hans-Georg Maassen Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Sohn

Ingawa hakusema wazi ni aina gani ya teknolojia na vifaa vilivyonunuliwa, Maassen amesema vilikuwa ni vifaa vyenye matumizi ya aina mbili yani vinaweza kutumika kwa ajili ya raia na pia kwa matumizi ya kijeshi.

"Tunapogundua kitu kama hicho, tunakizuia", alisema Maassen akiongeza kwamba "lakini hatuwezi kutoa uhakikisho kwamba tutaweza kugundua kila kitu na kuzuia visa vyote".

Maassen pia alibainisha kwamba sehemu ya mpango wa Pyongyang ulipatikana kupitia masoko mengine au kwamba makampuni hewa yanaweza kuwa yamepata nchini Ujerumani.

Shirika hilo la BfV liliweza kubaini taarifa za ugavi wa Korea Kaskazini mwaka 2016 na 2017 kwa mujibu wa uchunguzi wa NDR. Vifaa hivyo vinaripotiwa kutumika katika mpango wa Korea kaskazini wa nyuklia. Mwaka 2014, mwanadiplomasia wa Korea Kaskazini alijaribu kununua kifaa cha "utambuzi wa gesi", ambacho kinatumika katika uzalishaji wa silaha za kemikali.

Ripoti ya vikwazo vya Korea Kaskazini

Nordkorea Raketentest in Pjöngjang
Picha ya kombora la masafa ya kati kama ilivyotolewa na Korea Kaskazini Picha: Getty Images/AFP/STR

Tuhuma hizo za BfV zinafuatia ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa kwamba Korea Kaskazini imekuwa ikikiuka vikwazo. Umoja wa Mataifa ulibaini kwamba nchi hiyo imeendelea kusafirisha makaa ya mawe, chuma na bidhaa nyingine ambazo zimepigwa marufuku na kujipatia mapato ya karibu yuro milioni 160.

Korea Kaskazini iliuzia Myanmar mfumo wa makombora ya masafa marefu na huenda inaisaidia Syria na mpango wa silaha za kemikali kwa mujibu wa ripoti hiyo. Kwa miaka kadhaa, Umoja wa Mataifa umekuwa ukizidisha vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Iddi Ssessanga