1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini na Kusini zajadili kuhusu mkutano wa kilele

Grace Kabogo
6 Machi 2018

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amekutana na ujumbe wa Rais wa Korea Kusini Moon Jae-In na kujadiliana juu ya uwezekano wa kuandaa mkutano wa kilele kati ya nchi hizo zilizokuwa zikihasimiana kwa miaka kadhaa.

https://p.dw.com/p/2tkuR
Nordkorea Kim Jong Un mit südkoreanischer Delegation
Picha: picture-alliance/Newscom/KCNA

Ujumbe huo wa Korea Kusini ndiyo wa ngazi ya juu kabisa kuizuru Korea Kaskazini kwa zaidi ya muongo mmoja na ziara hiyo inafanyika wakati ambapo Rais Moon anajaribu kuongoza mazungumzo kati ya Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia na Marekani baada ya miezi kadhaa ya mvutano mkali.

Ziara hiyo ni hatua ya hivi karibuni kuhusu juhudi zilizoanzishwa wakati wa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mwezi uliopita wa Februari, kwa lengo la kuimarisha uhusiano katika Rasi ya Korea ambayo imegawanyika. Shirika la habari la Korea Kaskazini, KCNA limesema pande zote mbili zilifanya mazungumzo na kufikia makubaliano ya kuandaa mkutano wa kilele kati ya viongozi wa ngazi ya juu wa nchi hizo mbili.

Nordkorea Kim Jong Un spricht mit südkoreanischer Delegation
Kim Jong Un akisalimiana na ujumbe wa Korea KusiniPicha: picture-alliance/dpa/KCNA

Kwa mujibu wa shirika la KCNA, wakati wa chakula cha usiku hapo jana, Kim alielezea nia yake ya ''kuandika historia mpya ya kuungana tena kwa taifa hilo.'' Picha zilimuonyesha Kim mwenye furaha wakati akipokea barua kutoka kwa Moon na akipeana mikono na kiongozi wa ujumbe huo huku akitabasamu.

Hata hivyo, Korea Kusini imesema hakuna makubaliano yoyote ambayo yamefikiwa kuhusu mkutano huo kati ya Kim na Moon, ambao utakuwa wa kwanza wa aina hiyo kufanyika tangu mwaka 2007. Msemaji wa Ikulu ya Korea Kusini, Blue House, Kim Eui-Kyeom amethibitisha kuwa pande hizo mbili zimejadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu masuala kadhaa.

Mkutano ulidumu kwa saa nne

''Ujumbe wetu wa maafisa watano umekutana na Kim Jong Un pamoja na kamanda wa jeshi la Korea Kaskazini na mazungumzo yao yamechukua muda wa saa nne na dakika 12 na Kim alikabidhiwa barua binafsi kutoka kwa Moon,'' amesema Eui-Kyeom

Ujumbe wa watu watano kutoka Korea Kusini, akiwemo mshauri mkuu wa masuala ya usalama wa Rais Moon, ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe huo, Chung Eui Yong, ulikutana na Kim pamoja na viongozi wengine wa Korea Kaskazini mjini Pyongyang. Hiyo ni mara ya kwanza kwa Kim kukutana na maafisa wa Korea Kusini tangu alipoingia madarakani mwaka 2011.

Nordkorea Hwasong-14 Test
Kombora la Korea KaskaziniPicha: Getty Images/AFP/KCNA

Rais Moon amesema lazima wazungumze na Korea Kaskazini kuhusu kuachana na silaha za nyuklia katika Rais ya Korea. Korea Kaskazini na Marekani zote zimesema ziko tayari kufanya mazungumzo, lakini msimamo wa Marekani umekuwa ukisisitiza lengo la Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa nyuklia, hatua ambayo nchi hiyo imekuwa ikikataa.

Korea Kaskazini imesisitiza kwamba mazungumzo ya amani yanapaswa kuanza bila ya kuwepo masharti yoyote yale, na imelipuuza sharti hilo la Marekani.

Ujumbe wa Korea Kusini tayari umerejea nyumbani baada ya kukamilika kwa ziara hiyo ya siku mbili kwa ujumbe huo kukutana na wawakilishi wa Korea Kaskazini.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, AFP, DW http://bit.ly/2FfKhKB
Mhariri: Mohammed Abudl-Rahman