1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yaonyesha nguvu zake za kijeshi

Grace Kabogo
8 Februari 2018

Korea Kaskazini imefanya gwaride kubwa la kijeshi kuadhimisha miaka 70 tangu lilipoanzishwa jeshi la nchi hiyo, siku moja kabla ya kufunguliwa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi katika nchi jirani ya Korea Kusini.

https://p.dw.com/p/2sJaB
Nordkorea Militärparade Symbolbild
Picha: Getty Images/AFP/E. Jones

Korea Kaskazini imefanya gwaride kubwa la kijeshi kuadhimisha miaka 70 tangu lilipoanzishwa jeshi la nchi hiyo, siku moja kabla ya kufunguliwa kwa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi katika nchi jirani ya Korea Kusini.

Afisa wa Korea Kusini ambaye hakutaka kutajwa jina amesema kiasi ya wanajeshi 13,000 wameshiriki katika gwaride hilo lililokuwa na lengo la kuonesha nguvu ilizonazo Korea kaskazini na lililofanyika mapema leo asubuhi katika mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang. Watu wapatao 50,000 wamehudhuria gwaride hilo. Waandishi wa habari wa kigeni hawakualikwa katika gwaride hilo.

Gwaride hilo limekuwa likifanyika kila mwezi Aprili, lakini hivi karibuni tarehe hiyo ikabadilishwa na kutangazwa kuwa tarehe ya kufanyika kwa gwaride la kijeshi itakuwa Februari 8. Haikufahamika wazi kama kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amehutubia katika gwaride hilo kama alivyofanya kwenye matukio megine makubwa ya awali ya nchi hiyo. Aidha, halijaonyeshwa moja kwa moja katika televisheni ya taifa.

Nordkorea Militärparade
Wanajeshi wa Korea Kaskazini wakipiga saluti wakati wa gwaride Picha: picture-alliance/AP Photo

Korea Kusini imesema haijulikani iwapo Korea Kaskazini iliweka silaha nzito nzito kama vile makombora ya masafa marefu wakati wa gwaride hilo. Gwaride kubwa nchini Korea Kaskazini lilifanyika mwezi Aprili mwaka uliopita wakati wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa taifa hilo, Kim Il Sung.

Wakati huo huo, Korea Kaskazini imesema haina mpango wa kukutana na maafisa wa Marekani wakati wa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi itakayoanza kesho Korea Kusini. Tangazo hilo limetolewa leo, siku moja baada ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence kusema kuwa yuko tayari kukutana na maafisa wa Korea Kaskazini wakati wa sherehe za ufunguzi wa michezo hiyo.

Korea Kaskazini: Hatujaomba mazungumzo na Marekani 

Afisa mwandamizi katika wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini, Cho Yong-Sam amesema hakuna mpango kama huo na hawajawahi kuomba kufanyika kwa mazungumzo yoyote na Marekani na hawawezi kufanya hivyo.

Awali Pence alikataa kusema iwapo kutakuwa na mkutano kati ya nchi hizo mbili, lakini jana aliikosoa Korea Kaskazini na kutangaza kuwa Marekani itaweka vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo, kama hatua ya kuishinikiza kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Israel US-Vizepräsident Pence vor Knesset in Jerusalem
Makamu wa Rais wa Marekani, Mike PencePicha: Reuters/A. Schalit

''Na kama nilivyosema jana, tutaendelea na kampeni hii ya kuishinikiza Korea Kaskazini hadi itakapoachana kabisa na mpango wake wa nyuklia pamoja na makombora,'' alisema Pence. Makamu huyo wa rais wa Marekani amewaambia waandishi habari kwamba hawatoruhusu propaganda za Korea Kaskazini kuiharibu michezo hiyo ya Olimpiki wakati wa majira ya baridi.

Afisa anayeongoza ujumbe wa Korea Kaskazini kwenye michezo hiyo, Kim Yong-Nam pamoja na Pence wanatarajiwa kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa michezo hiyo. Dada wa Kim, Kim Yo Jung pia atahudhuria sherehe hizo. Pence ambaye tayari amewasili Korea Kusini atakutana na Rais Moon Jae-in kumshinikiza kuweka msimamo imara dhidi ya Korea Kaskazini yenye silaha za nyuklia.

Ama kwa upande mwingine, Rais Moon pia atakutana na kula chakula cha mchana na dada wa Kim pamoja na wajumbe wengine wa Korea Kaskazini wanaohudhuria sherehe hizo siku ya Jumamosi. Moon anaichukulia michezo hiyo kama fursa ya kufungua uhusiano wa kidiplomasia kati ya Korea hizo mbili, hatua ambayo Pence anaichukulia kwa tahadhari kubwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba