1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yarusha kombora la masafa marefu

Caro Robi
29 Novemba 2017

Korea Kaskazini imesema imefanikiwa kufanya jaribio la kombora la masafa marefu ambalo lina nguvu ya kushambulia eneo lolote Marekani.

https://p.dw.com/p/2oQwA
Nordkorea Raketentest in Pjöngjang
Picha: Getty Images/AFP/STR

Jaribio hilo ndilo la kwanza kurushwa na Korea Kaskazini tangu mwezi Septemba na linakuja wiki moja baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuiweka nchi hiyo katika orodha ya nchi zinazotajwa kuuunga mkono ugaidi.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani James Mattis amesema kombora hilo la hivi punde limeruka umbali mrefu zaidi na hivyo kumaanisha kuwa Korea Kaskazini inazidi kujiimarisha katika majaribio yake ya makombora. Kombora hilo la masafa marefu linasemekana kuruka juu na mbali zaidi kuliko makombora yaliyofanyiwa marekebisho kipindi cha nyuma.

Kombora lina nguvu kuliko yaliyopita

Kulingana na taarifa iliyosomwa katika kituo cha televisheni cha Korea Kaskazini, Kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong Un alishuhudia kurushwa kwa ufanisi kombora hilo lililopewa jina Hwansong 15 na kujivuna sasa wamekamilisha azma yao ya kihistoria ya kuwa dola lenye nguvu za kinyuklia.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akizungumza na maafisa kuhusu silaha za kinyuklia
Kiongozi wa Korea Kaskazini (Aliyesimama katikati) Kim Jong UnPicha: picture-alliance/AP/Korean Central News Agency

Kombora Hwangsong 15 lina nguvu mara mbili ya lile lililorushwa mwezi Julai mwaka huu. Kituo hicho cha habari KCNA kilisema kuwa kombora hilo liliruka urefu wa kilomita 4,475 na kusafiri kwa umbali wa kilomita 950 katika dakika 53 kabla ya kuanguka katika bahari karibu na Japan.

Nchi hiyo imesema inapenda amani na inaunda tu silaha za kinyuklia ili kujihami dhidi ya bepari Marekani na sera zake kandamizi za kinyuklia na vitisho vya mashambulizi ya kinyuklia kutoka kwa nchi hiyo.

Marekani, Japan na Korea Kusini zote zinakubaliana kuwa kombora hilo huenda ni la masafa marefu lakini wizara ya ulinzi ya Marekani imesema halikuwa kitisho kwa Marekani, maeneo wanayoyadhibiti wala washirika wake.

Trump na mwenzake wa Korea Kusini Moon Jae In wameonya kuwa kombora lililorushwa na Korea Kaskazini ni kitisho kikubwa kwa dunia. Baada ya Trump na Moon kuzungumza kupitia njia ya simu, Taarifa kutoka kwa Ikulu ya Rais wa Marekani imesema viongozi hao wametilia mkazo kuwa uchokozi huo kutoka kwa Korea Kaskazini ni kitisho sio tu kwa Marekani na Korea Kusini, bali kwa ulimwengu mzima.

Trump asema wataishughulikia ipasavyo hali iliyojiri

Trump pia alizungumza na Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe kuhusiana na kitendo hicho cha Korea Kaskazini kurusha kombora licha ya kuwekewa vikwazo chungu nzima na Jumuiya ya kimataifa.

USA Präsident Donald Trump im Weißen Haus in Washington
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Getty Images/K. Dietsch-Pool

Japan na Korea Kusini zimetaka Korea Kaskazini kuwekewa shinikizo zaidi kuizuia kurusha makombora na kufanya majaribio ya silaha za kinyuklia. Marekani, Korea Kusini na Japan zimeitisha kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baadaye Jumatano kujadili mzozo huo wa Korea Kaskazini.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani kurushwa kwa kombora hilo na kuitaka Korea Kaskazini kujiuzuia kufanya vitendo vitakavyosababisha msukosuko. China imesema inatiwa wasiwasi mkubwa kutokana na kitendo cha Korea Kaskazini kurusha kombora na kutoa wito pande zote kuwa na uvumilivu ili kudumisha amani na uthabiti.

Trump amewaambia wanahabari kuwa wataishughulikia ipasavyo hali iliyojitokeza na kwamba utawala wake hautabadili msimamo wake dhidi ya Korea Kaskazini ikiwemo kutaka iwekewe vikwazo zaidi ambavyo vitaathiri biashara zake. Kiongozi huyo wa Marekani na wa Korea Kaskazini wamekuwa wakirushiana cheche kali za maneno kwa miezi kadhaa sasa.

Marekani mara kwa mara imesema itatumia njia zote ikiwemo ya kijeshi kuikabili Korea Kaskazini lakini imesisitiza kwa sasa inapenda kutumia njia ya kidiplomasia. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson amesema njia hiyo ya kidiplomasia bado iko wazi kwa sasa.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Mohammed khelef