1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea kaskazini yarusha roketi angani

7 Februari 2016

Korea Kaskazini imerusha roketi ya masafa marefu leoJumapili (07.02.2016) ikibeba kile ilichosema kuwa ni satalaiti, lakini majirani zake na Marekani zinashutumu kitendo hicho kuwa ni jaribio la kombora.

https://p.dw.com/p/1Hr1h
Nordkorea bereitet Start einer Weltraumrakete vor ARCHIV
Roketi ya Korea kaskaziniPicha: picture alliance/AP Photo/KCNA

Jaribio hilo kwa mujibu wa nchi jirani na Marekani limefanywa kwa kukaidi vikwazo vya Umoja wa Mataifa na wiki chache tu baada ya majaribio la bomu la nyuklia.

Kikosi cha mikakati cha jeshi la Marekani kimesema kiligundua kombora likiingia angani siku ya Jumapili (7 Februari) na jeshi la Korea Kusini limesema roketi limerushwa na kupeleka kitu katika anga la juu, ikifuta ripoti za hapo kabla za vyombo vya habari kwamba roketi hiyo imeharibika wakati ikirushwa angani.

Nordkorea startet Weltraumrakete
Korea kaskazini ikionesha kurushwa kwa roketiPicha: Reuters/K. Hong-Ji

Bado ni mapema mno kuthibitisha

"Kila kitu tulichokiona ni sawa na kilichofanywa kwa mafanikio mwaka 2012," amesema mtaalamu wa teknolojia ya makombora wa Marekani John Schilling, akielezea kuhusu urushaji wa hapo kabla wa kile Korea kaskazini ilichosema kuwa ni satalaiti ya mawasiliano.

"Lakini bado ni mapema mno kusema kwa hakika," amesema Schilling, ambaye anahusika katika mradi unaojulikana kama "Kaskazini 38" unaangalia shughuli za Korea kaskazini katika chuo kikuu cha Hopkins.

Roketi hilo lilirushwa majira ya asubuhi saa za Korea likielekezwa upande wa kusini. Kituo cha televisheni cha Japan cha Fuji kimeonesha mstari wa mwanga ukielekea angani, ambapo picha hizo zilichukuliwa kutoka katika kamera zilizoko mpakani mwa China na Korea kaskazini.

Korea kaskazini, ambayo mwezi uliopita iliripua kile kilichoelezwa kuwa ni bomu la nyuklia, iliyafahamisha mashirika ya Umoja wa Mataifa kwamba inapanga kurusha roketi ikibeba satalaiti ambayo itakuwa inachunguza sayari yetu ya dunia, na kuzusha upinzani kutoka serikali mbali mbali ambazo zinaona hatua hiyo kuwa ni jaribio la kombora la masafa marefu.

Sohae Nordkorea Raketenbasis Raketenabschuss Station
Eneo lililorushiwa roketi hiyoPicha: picture-alliance/dpa

Televisheni ya taifa ya Korea kaskazini imesema inapanga kutoa , "taarifa rasmi" saa za mchana.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliripotiwa huenda lingefanya kikao cha dharura siku ya Jumapili (07.02.2016) kujadili hatua hiyo ya Korea kaskazini kurusha roketi, kwa ombi la Marekani, Japan na Korea kusini, wanadiplomasia wamesema.

Korea kaskazini ambayo imetengwa hapo awali ilitoa tarehe ya Februari 8 - 25 kwa ajili ya kurusha roketi hiyo lakini Jumamosi ilibadili na kuwa Februari 7 - 14, na kuchukua fursa ya hali ya hewa nzuri siku ya Jumapili.

Marekani kufanyakazi na Umoja wa Mataifa kuhusu Korea Kaskazini

Marekani ilikuwa inafuatilia kurushwa huko kwa roketi na kusema haikuamini kwamba hatua hiyo ilikuwa inaleta kitisho kwa Marekani ama washirika wake, afisa wa wizara ya ulinzi amesema.

USA Kerry beim IS Außenministertreffen in Rom
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John KerryPicha: Reuters/N. Kamm

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema Marekani itafanyakazi pamoja na baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuhusu "hatua maalum" kuiwajibisha Korea kaskazini kutokana na kurusha roketi hiyo.

Akikiita kitendo cha kurusha roketi hiyo ukiukaji mkubwa wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa katika matumizi ya nchi hiyo ya teknolojia ya silaha za makombora, Kerry alirudia kile alichosema kuwa ni "nguo ya chuma" ya dhima ya ulinzi ya Marekani kwa washirika wake Japan na Korea kusini na kuiita hatua hiyo ya kurusha roketi kuwa inaleta hali ya wasi wasi na ni changamoto isiyokubalika kwa amani na usalama.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Mohammed Khelef