1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kusini na Kaskazinitayari kwa mazungumzo

Caro Robi
2 Januari 2018

Korea Kusini imesema iko tayari kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Korea Kaskazini. Msimamo huo umeelezwa baada ya Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kusema yuko tayari kufanya mazungumzo na Korea Kusini.

https://p.dw.com/p/2qCqK
Nordkorea Kim Jong Un
Picha: Reuters/KCNA

Licha ya kuwepo mzozo wa silaha za kinyuklia, Korea Kusini imesema mazungumzo ya ngazi ya juu ya pande hizo mbili yanatarajiwa kufanyika Jumanne wiki ijayo na ni suala ambalo imelijadili na Marekani.

Uamuzi kuhusu iwapo Marekani na Korea Kusini zitasitisha kwa muda mazoezi ya pamoja ya kijeshi hadi kukamilika kwa mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi yatakayoandaliwa Korea Kusini bado haujaamuliwa.

Hali ya taharuki imekuwa ikiongezeka kutokana na mpango wa Korea Kaskazini wa kufanyia majaribio silaha za kinyuklia na kurusha makombora licha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha maazimio kuitaka nchi hiyo kusitisha mpango wake huo na kuiwekea vikwazo chungu nzima kwa kukiuka maazimio hayo.

Je mahusiano yataimarika?

Cheche za maneno makali na vitisho kutoka kwa kiongozi wa Korea Kaskazini na wa Marekani Donald Trump, zimedisha hata zaidi wasiwasi wa hatari ya matumizi ya silaha za kinyuklia. Trump ameapa kuiangamiza kabisa Korea Kaskazini iwapo itathubutu kuishambulia Marekani.

Südkorea Cho Myong Gyon, Vereinigungsminister
Waziri wa muungano wa Korea Kusini Cho Myoung-GyonPicha: Getty Images/AFP/J. Yeon-Je

Korea Kaskazini inataka jirani yake Korea Kusini kusitisha mazoezi ya kijeshi na Marekani ambayo inayatizama kama maandalizi ya kuingia vitani.

Waziri wa masuala ya muungano wa Korea Kusini Cho Myong-gyon amewaambia wanahabari kuwa wanasubiri kwa hamu kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wenzao wa Korea Kaskazini katika kijiji kilichoko mpakani cha Panmunjom na pia kujadili suala la nchi hiyo kushiriki katika mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi yanayotarajiwa mwezi ujao miongoni mwa masuala mengine kama Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa kinyuklia.

Cho aliongeza kuwa serikali ya Korea Kusini iko wazi kufanya mazungumzo na Korea Kaskazini wakati wowote, mahali popote na kwa namna yoyote. Iwapo mazungumzo hayo yatafanyika tarehe tisa wiki ijayo, yatakuwa mazungumzo ya kwanza ya ngazi ya juu kati ya nchi hizo mbili tangu yale yaliyofanyika Desemba mwaka 2015.

Matumaini hayo ya kuimarika kwa mahusiano kati ya Korea hizo mbili yanakuja baada ya hotuba ya Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ya kuukaribisha mwaka mpya ambapo alisema yuko tayari kwa mazungumzo na Korea Kusini na kuwa wanamichezo wa nchi yake huenda wakashiriki katika mashindano ya Olimpiki lakini akasisitiza kuwa nchi yake inalenga kuwa na nguvu kubwa ya kinyuklia.

China imesema kauli hizo kutoka kwa Korea Kaskazini na Korea Kusini za kutaka kuimarisha mahusiano kati yao zinapokelewa vyema kwani ni jambo zuri litakalopelekea kuepusha mzozo katika rasi ya Korea na hatimaye kuachana na mpango wa kuunda silaha za kinyuklia.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/dpa

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman