1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kusini yasema tamaa ya mazungumzo na Taliban ipo

7 Agosti 2007

Korea Kusini ina matumaini makubwa ya kufanyika mazungumzo ya pamoja na wateka nyara wa kundi la Taliban wanaowashikilia raia wake 21 hasa kutokana na kuzungumza na mmoja wa mateka hao kwa njia ya simu.

https://p.dw.com/p/CHjs
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan
Rais Hamid Karzai wa AfghanistanPicha: PA/dpa

Wapatanishi wa Korea Kusini walio nchini Afghanistan walifanikiwa kuzungumza na mmoja wa mateka 21 raia wa Korea Kusini wanaoshikiliwa na kundi la Taliban kwa mujibu wa ubalozi wake nchini Afghanistan.

Hata ingawa mazungumzo yalikuwa mafupi ubalozi huo umesema hautatowa maelezo zaidi kwa kuzingatia usalama wa raia wake.

Kundi la Taliban liliwateka nyara raia 23 wa Korea Kusini wafanyakazi wa kanisa mnamo julai 19 na mpaka sasa wawili kati ya mateka hao wamesha uwawa katika jitihada za kuilazimisha serikali ya Afghanistan itekeleze madai ya kuwaachilia huru wafungwa wafuasi wa kundi hilo.

Kundi la Taliban lilikuwa linasubiri yale yatakayojiri katika mkutano baina ya rais George Bush wa Marekani na mshirika wake rais Hamid Karzai wa Afghanistan.

Lakini matokeo ya mkutano huo ni kuwa viongozi hao wamekataa kata kata kutolewa ridhaa ya aina yoyote ile kwa kundi hilo la Taliban ambalo rais Karzai amelitaja kuwa sio tishio kwa serikali yake.

Rais Bush amelitaka kundi hilo liwaachilie mateka hao wa Korea Kusini kwa haraka.

Msemaji wa Taliban Yousouf Ahmadi amesema kwamba wapatanishi wa Korea Kusini awali waliwahakikishia kwamba rais Roh Moo-Hyun wa Korea Kusini alimuomba rais Bush msaada juu ya kuachiliwa wafungwa wa Kitaliban ili raia wake waachiwe huru bwana Ahmadi amesema, Bush na Karzai ndio watakao beba jukumu kwa lolote litakalo tokea.

Marekani ilihusika katika mpango wa kuachiliwa wafungwa wa Kitaliban mwezi Machi ambao uliwezesha kuachiliwa mwanahabari raia wa Italia na kuuwawa kwa kukatwa vichwa dereva na mkalimani wake raia wa Afghanistan na hapo rais Karzai aliapa kuwa hakutatokea tena makubaliano ya aina hiyo.

Msemaji huyo wa kundi la Taliban ameongezea kusema kwamba matamshi hayo ya rais Karzai hayabadilishi chochote na kwamba utekaji nyara utaendelea kama kawaida.

Jamii ya kimataifa pamoja na viongozi wa kiislamu wamelaani kitendo cha kutekwa nyara raia hao wa Korea Kusini wakiwemo wanawake 16.

Maandamano yamefaynika katika mji wa kusini wa Kandahar nchini Afghanistan, takriban watu 300 walizunguka ndani ya magari ya aina ya Pick Up wakidai mateka wa Korea Kusini waachiwe huru na kuwalaani watekaji nyara hao.

Mjini Seoul nchini Korea Kusini makundi ya wanaharakati wameandamana kuitaka Marekani iingilie kati ili wafungwa wa Kitaliban waachiwe kwa ajili ya kunusuru maisha ya raia 21 wa Korea Kusini.