1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korti ya katiba yasema chama cha NPD hakina madhara

Oumilkheir Hamidou
18 Januari 2017

Uamuzi wa korti ya katiba kupinga kupiga marufuku chama cha siasa kali za mrengo wa kulia NPD na jinsi waziri mkluu Theresa May avyopanga kuitoa Uingereza katika Umoja wa ulaya au Brexit-magazetini

https://p.dw.com/p/2VyFR
Bundesverfassungsgericht in Karlsruhe
Picha: picture-alliance/dpa/U. Deck

Tunaanzia lakini Karlsruhe na uamuzi wa majaji wa korti ya katiba  kuhusu madai ya kupigwa marufuku chama cha siasa kali za mrengo wa kulia NPD. Maoni ya wahariri yanatofautiana kuhusu uamuzi huo kuna wanaounga mkono na wengine wasiokubaliana nao. Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Neue Presse anaandika: "Majaji wa mjini Karlsruhe wamepitisha uamuzi unaokubalika. NPD kimepoteza umuhimu wake kuweza kutishia mwongozo wa kidemokrasi. Lakini mwenye kufuata siasa kali za mrengo wa kulia, marufuku hayamshitui. Zaidi ya hayo wengi wameshajiunga na makundi mengine. Na hasa katika chama cha Chaguo Mbadala kwa Ujerumani-AfD. Zaidi ya hayo kuna vitisho vyengine pia vinavyoikaba demokrasia wakati huu tulio nao. Vitisho hivyo ni pamoja na mabishano yanayohanikiza katika mitandao ya kijamii . Yote hayo serikali inabidi ikabiliane nayo kwa nguvu. Na kuhusu NPD watu wanabidi wafuate ile njia iliyotajwa na korti ya katiba: yaani namna chama hicho cha siasa kali kinavyogharimiwa na kuona kama njia hizo zinaweza kufungwa."

Kitisho cha NPD kingalipo

Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linahisi kitisho cha NPD bado hakijatoweka. Gazeti linaendelea kuandika: "Majaji wa korti ya katiba wamewaondoa patupu wanasiasa,.taasisi na serikali-na wameipoteza fursa ya kihistoria. Kwasababu hata kama "maeneo yaliyokombolewa ya taifa", ambayo NPD wanasema wamevitimua vyama vya kidemeokrasi, si mengi, hata hivyo yapo-yanakutikana Meckelnburg-Vorpommern, Saxony na sehemu nyengine za mashariki ya Ujerumani. Viongozi wengi wa NPD walijiweka kando kesi ilipokuwa inaendelea, sasa lakini wataanza upya kujitokeza. Watazidisha makali ya siasa zao za kibaguzi na kugeuka kitovu cha wanazi mambo leo-hali inayoashiria kuwa ya hatari kupita kiasi."

Mtaka yote hukosa yote

 Mada ya pili iliyohanikiza magazetini inahusu hotuba ya waziri mkuu wa Uingereza Theresa May aliyefafanua jinsi nchi yake inavyopanga kujitoa katika Umoja wa Ulaya. Gazeti la mjini Cologne "Kölner Stadt Anzeiger" linaandika: "Hotuba ya Theresa May imepindukia makadirio yote. Waziri mkuu amechagua kuitoa nchi yake kwa kishindo toka Umoja wa Ulaya. Hoja zake zinalingana na zile za wanaoupinga Umoja wa ulaya mfano wa chama cha Ukip: Ikitoka katika Umoja wa ulaya, nchi hiyo haitoweza kusalia katika soko la pamoja. Hoja hizo licha ya kurudiwa kila mara, hazina msingi. Katika umoja wa forodha London inataka  kubakia kwa njia moja au nyengine, lakini haitaki kushiriki katika ulinzi wa pamoja wa mipaka ya nje - eti kwasababu wanataka kushirikiana na kila mmoja na kufikia makubaliano ya kibiashara na mataifa ya nje. Badala ya kupunguza madhara yanayotokana na Brexit, waziri mkuu Theresa May anazidi kuvuruga mambo. Na waingereza watapata shida kubwa chini ya uongozi wake."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman