1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kroos ayafufua matumaini ya Ujerumani

24 Juni 2018

Kiungo wa kati wa Ujerumani Toni Kroos alifunga goli katika dakika ya tano ya muda wa ziada na kuwapa Ujerumani ushindi wa 2-1 walipokuwa wakicheza na Sweden katika mechi yao ya pili ya Kundi F kwenye Kombe la Dunia.

https://p.dw.com/p/30AGO
WM Russland 2018 I Deutschland vs Schweden - Toni Kroos
Picha: picture-alliance/AP/F. Augstein

Ujerumani walikuwa wanahitaji angalau sare kwenye mechi hiyo ili wayaweke hai matumaini yao ya kufuzu kwenye hatua ya mtoano baada ya kulazwa na Mexico kwenye mechi ya kwanza.

Kroos ambaye ameshambuliwa na wachambuzi kwa kutoiongoza Ujerumani baada ya kustaafu kwa Bastian Schweinsteiger na Philip Lahm, alijitokeza katika hizo sekunde za mwisho za mechi ili apige mkwaju wa frikiki ambao walipewa Ujerumani baada ya Timo Werner kuangushwa upande wa kushoto nje ya eneo la hatari.

Huku mechi ikiwa sare ya 1-1 Kroos alimuanzia pasi fupi Marco Reus ambaye alimsimamishia mpira na kumpa nafasi ya kuipiga frikiki hiyo kwa utaalam na kuwapa goli la ushindi mabingwa hao watetezi wa dunia.

Kroos alitoa pasi mbaya iliyopelekea Sweden kuingia uongozini

Mapema kiungo huyo wa kati anayeichezea Real Madrid alikuwa ametoa pasi mbaya iliyopelekea Sweden kufunga goli lao katika dakika ya 32 kupitia kwa Ola Toivonen.

Russland WM 2018 Deutschland gegen Schweden
Toni Kroos akiwafungia Ujerumani goli la pili katika sekunde za mwishoPicha: Reuters/

Ujerumani walikuwa wanacheza na wachezaji kumi uwanjani baada ya Jerome Boateng kuondolewa uwanjani alipoonyeshwa kadi ya pili ya njano kwenye dakika ya 82 ya mechi alipomchezea vibaya mshambuliaji wa Sweden Marcus Berg. Mapema kwenye kipindi hicho cha pili Boateng alikuwa ameonyeshwa kadi ya kwanza ya njano.

Iwapo Ujerumani wangeshindwa mechi hii ingemaanisha kwamba wameondolewa mapema kwenye hatua ya makundi katika Kombe la Dunia na ni jambo ambalo lingekuwa limefanyika kwa mara ya kwanza kwa taifa hilo lenye ufuasi mkubwa wa mchezo wa mpira tangu mwaka 1938.

Ujerumani watahitajika wawashinde Korea Kusini Jumatano

Kocha wa Die Mannschaft, Joachim Löw alifanya mabadiliko kwenye kikosi chake kilichoanza mechi hiyo kwa kumuacha nje Mesut Özil, Sami Khedira na Mats Hummels ambaye alikuwa na jeraha la shingo. Nafasi zao zilichukuliwa na Marco Reus, Sebastian Rudy na Anthony Rudiger.

WM Russland 2018 I Deutschland vs Schweden - Toni Kroos
Toni Kroos akisherehekea na Anthony RudigerPicha: Reuters/M. Dalder

Ujerumani sasa watahitaji kushinda mechi yao ya mwisho ya makundi Jumatano watakapocheza na Korea Kusini ambao wana nafasi kubwa ya kuyaaga mashindano hayo baada ya kufungwa na Mexico 2-0. Lakini vijana hao wa Löw watahitaji pia Mexico ambao wanahitaji sare tu ili kutinga hatua ya mtoano, wawafunge Sweden.

Kwa sasa Mexico wanaongoza kundi hilo F wakiwa na pointi 6 kisha Ujerumani na Sweden wana pointi 3 kila mmoja halafu Korea Kusini ndiyo timu iliyo mkiani bila pointi yoyote.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/APE
Mhariri: Sekione Kitojo