1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KUALA LUMPUR:Mjumbe wa UN kurudi tena Myanmar mwezi ujao

17 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Ez

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa Ibrahim Gambari anatangaza kuwa atazuru tena nchi ya Myanmar mwezi ujao huku akijaribu kutafuta suluhu ya kidemokrasia. Kulingana na Bwana Gambari ni muhimu kukutana na kiongozi wa utawala wa kijeshi Jenerali Than Shwe aidha Bi Aung San Suu Kyi mshindi wa tuzo la Nobel anayetumikia kifungo cha nyumbani mjini Yangon.

Mjumbe huyo alikutana na viongozi wote wawili mwezi jana alipozuru Myanmar ili kuwakilisha jamii ya kimataifa kufuatia hatua ya serikali ya kuvamia waandamaanaji wanaodai demokrasia.Maandamano hayo yaliongozwa na watawa wa Kibudda na kusababisha vifo vya watu 13.

Ibrahim Gambari anakutana na viongozi wa Malaysia hii leo zikiwa ni juhudi za kuhusisha mataifa ya Asia ya Kusini mashariki kuzipa msukumo harakati za kutafuta demokrasia nchini Myanmar.Mjumbe huyo ananuia kuona mchango wa mataifa ya eneo hilo katika kutafuta suluhu ya tatizo la kisiasa la Myanmar kufuatia maandamano ya kudai demokrasia yaliyoongozwa na watawa wa Kibudda.

Utawala wa kijeshi wa Myanmar unakabiliwa na shinikizo kutoka jamii ya kimataifa tangu kushambulia waandamanaji wanaodai demokrasia katika maandamano ya mwezi jana.

Ziara ya Bwana Gambari ina lengo la kushinikiza uongozi wa kijeshi wa Myanmar kusitisha mashambulizi yake dhidi ya maandamano ya amani ya kudai demokrasia,kuachia wafungwa wa kisiasa aidha kuanzisha mazungumzo na vyama vya upinzani vinavyoongozwa na Aung San Suu Kyi.

Myanmar kwa upande wake inasisitiza kuwa haitashinikizwa na mataifa ya kigeni huku Japan ikisitisha msaada wake na Umoja wa Ulaya kuongeza vikwazo ilivyoiwekea.