1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kujiuzulu kwa kiongozi wa Cuba kulivyo karibishwa

Abdulrahman, Mohamed19 Februari 2008

Viongozi, nchi na jumuiya kadhaa dunia zimelikaribisha kwa maoni tafauti tangazo la kujiuzulu kiongozi wa Cuba Fidel Castro

https://p.dw.com/p/D9sm
Rais Castro anasema sababu kubwa ya kujiuzulu ni afya yake.Picha: picture-alliance/ dpa

Miongoni mwa viongozi ni Rais wa Marekani George Bush ambaye nchi yake kwa muda mrefu imekua ni hasimu mkubwa wa utawala wa Castro.

Akizungumza katika mji mkuu wa Rwanda-Kigali alikowasili leo kikiwa ni kituo cha tatu cha ziara yake barani Afrika, Rais George W.Bush wa Marekani alisema kwamba uamuzi wa Fidel Castro kuachia madaraka hauna budi kuwa mwanzo wa "kipindi cha mpito kuelekea demokrasia" nchini Cuiba ambacho hatimae kitafungua njia ya kuwepo kwa uchaguzi huru na wa hak. Hata hivyo Rais Bush hakuonyesha ishara yoyote ya mabadiliko katika sera za Marekani za karibu nusu karne sasa kuilekea jirani yake wa Kikoministi.

Kiongozi huyo wa Marekani alisema hatua ya kwanza ni kwa Cuba kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na kuitaka jamii ya kimataifa isaidie kujenga taasisi za demokrasia nchini Cuba, akiongeza kwamba Marekani nayo itasaidia.

Naye msemaji rasmi wa waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown amesema kuondoka Castro madarakani kunafungua njia ya kipindi cha amani cha mpito kuelekea demokrasia na kwamba hii sasa ni nafasi ya kupiga hatua kuelekea demokrasia ya vyama vingi.

Akaongeza kwamba pamoja na hayo kuna masuala yanayowahusu wananchi wa Cuba, akisisitiza kwamba kwa muda mrefu Uingereza imekua ikishajiisha kuwepo kwa demokrasia kisiwani Cuba na pia kuheshimiwa haki za binaadamu pamoja na kuachiwa huru bila masharti wafungwa wote wa kisiasa.

Waziri mkuu wa Denmark Anders Rasmussen ameupongeaza uamuzi huo wa Castro, akisema ni hatua inayoelekea njia inayofaa.

Nayo taarifa ya umoja wa ulaya mjini Brussels ilisisitiza juu ya haja sasa ya kufunguliwa njia kuelekea demokrasia nchini Cuba.


China imesema itaendeleza uhusiano wa kirafiki na Cuba ikimtaja kiongozi huyo wa kikoministi Fidel Castro kuwa rafiki wa siku nyingi wa umma wa nchi hiyo, wakati Vietnam amemtaja Castro kuwa " rafiki wa milele wa taifa hilo."

Akitangaza kuachia ngazi za utawala katika barua iliochapishwa na vyombo vya habari vya dola leo, Castro mwenye umri wa miaka 81 hakutaja ni nani anayemfikiria kuchukua nafasi yake .

Bunge la taifa litakutana Jumapili ijayo mjini Havana ambapo miongoni mwa mengine ni kupendekeza na kumchagua kiongozi wa baraza la taifa atakayekua moja kwa moja Rais mpya. Wachambuzi wanahisi huenda akawa ni ndugu yake Castro, Raul mwenye umri wa miaka 76 ambaye sasa ni waziri wa ulinzi akikaimu pia nafasi ya kiongozi wa taifa.

Tayari waziri wa uhispania anayeshughulikia masuala ya Amerika kusini Trinidad Jimenez amesema kujiuzulu kwa Castro kutamfungulia njia nduguye kushika nafasi hiyo, akisema itampa fursa Raul kuleta mageuzi, hasa kwa kuwa Raul Castro amezungumzia haja hiyo.

Shirika la kimataifa la haki za binaadamu limewataka viongozi wapya nchini Cuba kulainisha vikwazo dhidi ya haki za binaadamu nchini humo, huku likiitaka pia Marekani kumaliza hatua yake ya miongo kadhaa sasa ya vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Cuba.

Ama makundi ya upinzani yalioko nje yamesema hawaioni hatua ya Rais Castro kujiuzulu kuwa italeta madabiliko ya haraka, ikiwa hatamu zitashikwa na ndugu yake.

Rais Castro amesema sababu kubwa ya uamuzi wake wa kun´gatuka ni hali yake ya afya.