1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kujiuzulu kwa Sarrazin kwazua hisia tofauti

Josephat Nyiro Charo10 Septemba 2010

Kujiuzulu kwa Thilo Sarrazin, mwanachama wa bodi ya uongozi ya benki kuu ya Ujerumani kumezusha hisia mbalimbali humu nchini huku rais wa Ujerumani Christian Wulff akiepuka kibarua kipevu cha kumfuta kazi kiongozi huyo.

https://p.dw.com/p/P9Qq
Thilo Sarrazin akizindua kitabu chake hapo jana(09.09.2010) mjini PotsdamPicha: picture-alliance/dpa

Wanasiasa wa Ujerumani wamekukaribisha kujiuzulu kwa Sarrazin ambaye alizusha moto hapa Ujerumani kwa matamshi yake ya kibaguzi kuhusu rangi na dini. Sarrazin amesema ataacha wadhifa wake katika benki kuu ya Ujerumani, Bundesbank, mwisho wa mwezi huu. Kujiuzulu kwake kuna maana rais wa Ujerumani Christian Wullf hatalazimika kupitisha uamuzi mgumu wa kukubali au kukataa pendekezo la benki kuu kumtaka amfute kazi kiongozi huyo, uamuzi ambao ungetishia kumuweka kansela Angela Merkel katika kiti moto mbele ya wapigaji kura wa kihafidhina.

Rais Wullf amesema amekukaribisha kujiuzulu kwa Thilo Sarrazin na kwamba suluhisho la pamoja limefikiwa kwa ushirikiano na benki kuu ya Ujerumani.

Christian Wulff
Rais wa Ujerumani, Christian WulffPicha: picture alliance / dpa

Gazeti la Financial Times Deutschaland limeandika katika makala yake kwamba Sarrazin amejiangamiza mwenyewe, kama jina la kitabu chake kipya: Ujerumani yajiangamiza yenyewe. Kwa kujiuzulu Sarrazin amejiokoa yeye mwenyewe na Ujerumani nzima kutokana na mvutano wa kisheria ambao ungetokea kama angefutwa kazi.

Kwa mujibu wa maoni ya watu walioshiriki kwenye kipindi cha televisheni ya NTV cha kutoa maoni kwa njia ya simu, asilimia 89 ya watu waliopiga simu wamesema uamuzi wa Sarrazin kung´atuka ni kosa kubwa. Hata hivyo hisia za Wajerumani zimechanganyika katika barabara za mji wa Frankfurt, makao makuu ya benki kuu ya Ujerumani.

Chama cha Sarrazin cha SPD kimeanzisha mchakato wa kumfukuza chamani Sarrazin, ingawa matokeo ya kura ya maoni iliyofanywa hivi karibuni yanaonyesha kuwa hatua hiyo haitaungwa mkono na umma na wafuasi wa chama cha SPD wanaoamini chama hicho kinatakiwa kutumia muda wake kuyashughulikia masuala mengine muhimu zaidi.

Sebastian Edathy mwanachama wa SPD katika kamati ya masuala ya sheria ya bunge la Ujerumani, Bundestag, amesema kama Sarrazin amepitisha uamuzi huo kwa sababu ameona ukweli halisi wa mambo, basi bila shaka hatua muafaka anayopaswa kuchukua ni kukihama chama cha SPD bila vurugu.

Gazeti la Bild kwa upande wake limesema ni hatua ya kishujaa na ya kuwajibika kwa Sarrazin kujizulu, lakini inatoa picha mbaya kuhusu utamaduni wa kufanya mdahalo wa wazi hapa Ujerumani. Watetezi wanaopigania kuboreshwa kwa juhudi za kuwajumuisha wageni hapa Ujeruamani wanasema Sarrazin ameifanya kuwa vigumu kufanyika mdahalo wa maana kuhusu maoni yake na kuugubika ukweli wa madai yake yaliyozusha utata.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Othman Miraji