1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuku na mayai sumu tupu?

Abdu Said Mtullya5 Januari 2011

Maoni ya wahariri juu ya kugundulika mabaki za dizeli katika malisho ya kuku.

https://p.dw.com/p/ztmx
Mabaki ya dizeli yamegunduliwa katika chakula cha kuku
Mabaki ya dizeli yamegunduliwa katika chakula cha kukuPicha: Picture-Alliance/dpa

Wahariri wa magazeti leo wanazungumzia juu ya kashfa inayohusu sumu iliyogunduliwa katika chakula cha kuku. Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya neema iliyojitokeza katika soko la ajira nchini Ujerumani.

Mhariri wa Dresdner Neueste Nachrichten anatoa maoni yake juu ya Iran kwa kusema kuwa nchi hiyo imezialika zile nchi tu inazozitaka ziuone mpango wake wa nyuklia, na siyo yale mataifa ambayo kwa kawaida yanashiriki katika mazungumzo na nchi hiyo. Juu ya njama hizo mhariri wa gazeti hilo anasema licha ya kuzialika nchi inazozitaka, ni Iran peke yake inayojua hatua iliyoifikia katika utafiti wake wa nyuklia.Hata hivyo mhariri anasema anaetaka kuijua siri ya Iran anapaswa kuwa mbunifu. Kinachohitajika ni zaidi ya vikwazo.

Kiasi fulani cha dioxin-yaani mabaki ya dizeli, kimegunduliwa katika chakula cha kuku katika sehemu mbalimbali nchini Ujerumani. Dawa hiyo ni ya hatari kwani ina kiasi fulani cha sumu.

Juu ya kashfa hiyo mhariri wa Hannoversche Allgemeine anasema orodha ya kashfa zinazohusu sekta ya uzalishaji wa chakula ni ndefu nchini Ujerumani. Lakini orodha ya hatua zinazochukuliwa dhidi ya kashfa hizo ni fupi.Sasa watu nchini Ujerumani wameshazoea, kwani hakuna anaeamini kwamba mayai yote yatateketezwa madukani.Kwa viongozi, kazi itaendelea na hakuna anaeamini kwamba hatua zitachukuliwa ili kuwanasa wale wanaozalisha malisho ya mifugo kwa kutumia dawa zenye sumu kama dioxin.

Mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker pia haamini iwapo hatua zitachukuliwa dhidi ya wahalifu wanaozalisha chakula cha kuku kwa kutumia mabaki ya dizeli.Gazeti hilo linasema mara kwa mara pametokea kashfa katika sekta ya uzalishaji wa chakula kwa ajili ya mifugo nchini Ujerumani.Na kila mara idara zinazohusika zinatoa ahadi juu ya kuwachukulia hatua wahalifu, lakini mpaka sasa ahadi hizo hazijafuatiliwa na hatua zozote. Sababu ni kwamba viongozi wanagwaya , mara tu wanaomiliki sekta ya chakula cha wanyama wakisema kuwa nafasi za ajira zinaweza kuwa hatarini.Na matokeo yake ni kwamba hakuna kinachofanyika , hata baada ya kutokea kashfa.

Mhariri wa Mitteldeutsche anazungumzia neema iliyojitokeza katika soko la ajira nchini Ujerumani.Mhariri huyo anasema Ujerumani imefanikiwa kuukabili mgogoro mkubwa wa uchumi na kuibuka na nguvu kubwa.Lakini ustawi ulioleta nafasi zaidi za ajira unatokana pia na hatua kali.Hekima katika sera za ajira na za uchumi wakati wote zinaleta matunda.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mpitiaji: Josephat Charo