1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbkumbu za aina pekee kumwaga Helmut Kohl

Oumilkheir Hamidou
3 Julai 2017

Mada mbili kuu zimehanikiza magazetini: Mazishi ya kansela wa muungano na muasisi mmoja wapo wa Umoja wa Ulaya, Helmut Kohl, na hatua za usalama kuelekea mkutano wa kilele wa mataifa ya G-20 mjini Hamburg.

https://p.dw.com/p/2fov3
Straßburg Trauerfeierlichkeiten European Parliament Holds Helmut Kohl Memorial
Picha: Getty Images/S. Gallup

Tunaanzia na kumbukumbu za aina pekee zilizoandaliwa na Umoja wa Ulaya kumpa heshima za mwisho muasisi mmojawapo wa umoja huo, baba wa muungano wa Ujerumani Helmut Kohl. Kimsingi kiongozi wa serikali ya Ujerumani anapofariki dunia, linakuwa jukumu la serikali kuandaa kumbukumbu za kumpa heshima za mwisho naiwe katika ukumbi wa bunge la shirikisho au kwengineko. Safari hii na kwa mara ya kwanza alikuwa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker aliyeandaa kumbukumbu hizo kwa niaba ya Umoja wa ulaya. Licha ya manung'uniko, gazeti la "Berliner Zeitung" linaandika:"Ulikuwa uamuzi sahihi, kwa kumbukumbu za kumwaga Helmut Kohl kuandaliwa na Umoja wa Ulaya. Ni kumbukumbu zilizoandaliwa na bunge la Ulaya na sio na mtu mmoja. Na ulikuwa pia ujumbe wa kisiasa ambao umetekelezwa kwa heshima zote. Masaa mawili ya kumbukumbu mjini Strasbourg yalijaa jazba, lakini wito uliotolewa umeingia nyoyoni mwa walimwengu. Miongoni mwa  viongozi waliohudhuria ni pamoja pia na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anayetaka kuitoa nchi yake katika Umoja wa Ulaya na mwiba wa mchongoma wa Umoja wa Ulaya, waziri mkuu wa Hungary, Viktor Orban. Tutaraji tu kwamba wote hao wawili, na sio wao peke yao, wameupata ujumbe uliotolewa na kuwaingia nyoyoni mwao."

Changamoto za mkutano wa G-20 mjini Hamburg

Mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa 20 yanayoendelea na yaliyoendelea kiuchumi-G-20 unaanza Ijumaa ijayo katika mji wa kaskazini mwa Ujerumani, Hamburg. Tayari wanaharakati wameshaanza kuandamana licha ya hatua za usalama kuimarishwa. Gazeti la Hannovershe Allgemeine linaandika:"Jukumu la polisi ni tete, na nafasi waliyonayo ni ndogo. Hata hivyo wanaonyesha wako tayari kutekeleza jukumu lao hata kabla ya mkutano huo wa kilele kuanza. Kwa kutenga maeneo ya usalama ambayo ni marufuku kwa maandamano, polisi wanataka kubainisha kwa fakhari wanamiliki zana za kimambo leo za kiufundi na tathmini ya hukumu ya korti kuu ya mjini Karlsruhe iliyotolewa na maafisa wa serikali ya Hamburg imezidi kupalilia mambo. Ndo kusema wanataka kuwatisha wenye kutaka kufanya fujo au wanawahimiza? Wahka ni mkubwa pande zote mbili. Panahitajika kitu kidogo tu na maji yatazidi unga. Polisi watahitaji busara zaidi kuepusha balaa lisitokee. Na wanaoandamana kwa amani nao watabidi wajitenge na wale wenye kutaka kufanya fujo. La sivyo hakuna atakayelifikia lengo lake: Si mji wa Hamburg ambao kawaida unapenda kutuma picha za kuvutia ulimwenguni na wala si waandamanaji wanaotaka kubainisha hisia zao dhidi ya akina Trump, Putin au Erdogan.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Josephat Charo