1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kumbukumbu ya miaka 100 ya Verdun

30 Mei 2016

Viongozi wa Ujerumani na Ufaransa Jumapili (29.05.2016) wameshiriki kumbukumbu ya miaka 100 ya Mapambano ya Verdun kwa kuweka shada la maua katika makaburi ya wanajeshi 300,000 wa nchi hizo waliouwawa.

https://p.dw.com/p/1Iwgn
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Mapambano ya Verdun ni mojawapo ya mapambano yaliochukuwa muda mrefu katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia ambapo yalidumu kwa siku 300 kuanzia Februari hadi Disemba mwaka 1916. Mapambano hayo kaskazini mashariki ya Ufaransa licha ya kuwa makali kabisa na kugharimu maisha ya wanajeshi 163,000 wa Ufaransa na wanajeshi 143,000 wa Ujerumani yalishindwa kutowa mshindi.

Miongoni mwa matukio ya mwanzo ya kumbukumbu hiyo viongozi hao wa Ujerumani na Ufaransa waliweka shada la mauwa katika makaburi ya wanajeshi wa Ujerumani huko Consenvoye kaskazini mwa mji wa Verdun ambapo miili ya wanajeshi wa Ujerumani ilizikwa.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani walihudhuria hafla katika Ukumbi wa jiji huko Verdun ambapo katika hotuba yake Merkel amesema Verdun inasimamia sio tu "unyama usioelezeka na upuuzi wa vita " bali pia "kutowa mafunzo na usuluhishi wa Ujerumani na Ufaransa."

Mapambano ya Verdun ni funzo

Amesema "ni wale tu wanaojuwa kipindi cha kale wanaweza kujifunza kutokana na hayo na kutumia jambo hili kujenga mustakbali mwema" na kuongeza kwamba dhana ya urafiki aliyoipata katika mji huo akiwa kama kansela wa Ujerumani "haifai kabisa kuchukuliwa kijuu juu".

Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Yeye na Hollande pia walimkabidhi Meya wa Verdun Tuzo ya mwaka huu ya Adenauer - de Gaulle ambayo hutunukiwa wale wanaochangia kujenga uhusiano mzuri kati ya Ujerumani na Ufaransa.

Hollande amesema Verdun sio kitu kilichoganda na mahala pa kutukuzwa kwa wafu bali daima imekuwa ikiangalia mbele kwa matumaini kutimiliza lengo lake la amani.

Watoto wa Ufaransa na Ujerumani takriban 3,400 wamewasilisha igizo la halaiki la mapambano hayo katika uwanja wa makaburi huko Douaumont, ambapo miili ya wanajeshi 130,000 iliobakia kutoka pande zote mbili imezikwa.

Umuhimu wa Douaumont

Makaburi ya Douaumont yana umuhimu wake kwani ni mahala ambapo Kansela wa Ujerumani magharibi wa wakati huo Helmut Kohl na aliyekuwa Rais wa Ufaransa Francois Mitterand waliposhikana mikono wakati wa kumbukumbu ya mwaka 1984 ya vita hivyo ikiwa ni ishara ya kihistoria ya usuluhishi kati ya mataifa hayo mawili.

Aliyekuwa Kansela wa Ujerumani magharibi Helmut Kohl na rais wa zamani wa Ufaransa Francois Mitterand wakiwa Verdun 1984.
Aliyekuwa Kansela wa Ujerumani magharibi Helmut Kohl na rais wa zamani wa Ufaransa Francois Mitterand wakiwa Verdun 1984.Picha: ullstein bild/Sven Simon

Kumbukumbu ya mapambano hayo imekuja kuashiria uhusiano wa karibu uliopo kati ya Ufaransa na Ujerumani. Ni mwaka 1984 nchi hizo jirani ndipo zilipokubali kufanya hafla ya pamoja ya kumbukumbu ya mapambano ya Verdun ikiwa ni hatua nyengine mbele ya kukomesha uhasama na kutokuaminiana kati ya mataifa hayo mawili baada ya kumalizika kwa Vita Vikuu Viwili vya Dunia.

Mwaka huo pia ulishuhudia bunge la Ulaya likipitisha mkataba wa kuanzisha Umoja wa Ulaya na makubaliano kati ya Ufaransa na Ujerumani kuondowa ukaguzi wa mipaka hatua kwa hatua.

Changamoto kwa Umoja wa Ulaya

Akizungumza katika mkesha wa kumbukumbu hii Kansela Merkel amesema ukweli kwamba amealikwa kuhudhuria kumbukumbu hiyo mwaka huu ni ishara jinsi uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa ulivyo mzuri hivi sasa.

Wanafunzi wa Ufaransa katika warsha ya mapambano ya Verdun.
Wanafunzi wa Ufaransa katika warsha ya mapambano ya Verdun.Picha: Getty Images/AFP/J.-C. Verhaegen

Ujerumani na Ufaransa zinaonekana kuwa engini kuu ya Umoja wa Ulaya unaoundwa na mataifa wanachama 28 ambao hivi sasa unakabiliwa na changamoto kubwa kama vile wimbi la wahamiaji na wakimbizi wanaokimbilia Ulaya na misukosuko ya kifedha inayozikumba baadhi ya nchi wanachama.

Uwezekano wa kujitowa kwa Uingereza kutoka umoja huo umezidi kuongezea hisia iliozagaa kwamba umoja wa kundi hilo uko hatarini.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/dpa/AFP

Mhariri : Sudi Mnette