1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Sudan Omar al Bashir aitembelea Syria

Zainab Aziz
17 Desemba 2018

Rais wa Sudan Omar al Bashir ni kiongozi wa kwanza kutoka Umoja wa nchi za Kiarabu kuitembelea Syria tangu nchi hiyo itumbukie kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vya karibu miaka minane iliyopita

https://p.dw.com/p/3AEYI
Der syrische Präsident Bashar Assad mit dem sudanesischen Präsidenten Omar al-Bashir in Damaskus, Syrien die Hand
Picha: picture-alliance

Al-Bashir alipokelewa kwenye uwanja wa ndege wa Damascus na mwenyeji wake rais wa Syria Bashar Assad kabla ya viongozi hao kuelekea ikulu ambapo walifanya mazungumzo juu ya mahusiano ya nchi hizo mbili na maendeleo ya Syria pamoja na ya kanda ya mashariki ya kati.

Syria ilifukuzwa uanachama wa mataifa 22 ya Umoja wa nchi za Kiarabu baada ya kuanza vita vya mwaka 2011. Nchi za Kiarabu zimeiwekea nchi hiyo vikwazo na mara kwa mara zimekuwa zikimlaumu Assad kwa kutumia nguvu kubwa ya kijeshi na pia kushindwa kwake kujadiliana na wapinzani.

Sababu hasa ya ziara ya rais wa Sudan al-Bashir haijawekwa wazi lakini kutokana na kuwa vita vya nchini Syria vinaelekea ukiongoni kwa vikosi vya Assad kuwa kifua mbele, baadhi ya viongozi wa Kiarabu wameonyesha azma ya kutaka kurejesha mahusiano yao na serikali ya Syria.

Mnamo mwezi Oktoba, Bashar al Assad aliliambia gazeti moja la Kuwaiti ambalo halijulikani sana kuwa Syria ina maafikiano na baadhi ya nchi za Kiarabu baada ya miaka mingi ya uadui kati yao licha ya kwamba hakuzitaja nchi hizo za Kiarabu katika mahojiano hayo. Assad pia alifahamisha kuwa wajumbe wa Kiarabu na wa nchi za Magharibi wameanza kuitembelea Syria ili kufanya maandalizi ya kufungua balozi na ofisi nyinginezo.

Kushoto: Rais wa Sudan Omar al Bashir Kulia: Rais wa Syria Bashar al Assad
Kushoto: Rais wa Sudan Omar al Bashir Kulia: Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: picture-alliance

Mahojiano hayo yalifuatia mkutano wa kushangaza uliokuwa wa kirafiki kati ya waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid Muallem, na mwenzake wa Bahrain Khalid bin Ahmed Al Khalifa, uliofanyika kandoni mwa mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi Septemba huko mjini New York. Mkutano huo uligeuza vichwa vingi hasa mawaziri hao walipooneka wakipigana pambaja tena kwa furaha.

Kwa mujibu wa maafisa wa Sudan rais Al bashir alirejeaa Khartoum jana jioni mara baada ya kumaliza mazungumzo na mwenyeji wake mjini Damascus. Rais wa Sudan mara ya mwisho aliutembelea mji huo mkuu wa Syria mnamo mwaka 2008 alipohudhuria mkutano wa Umoja wa nchi za Kiarabu uliofanyika huko mwaka huo.

Zaidi ya watu 360,000 wameuwawa kwenye vita vya nchini Syria na mamilioni wengine wameyakimbia makazi yao tangu vilipoanza vita hivyo mnamo mwaka 2011. Vita hivyo vimesababisha mgogoro mkubwa unaohusisha makundi ya kijihadi ikiwa ni pamoja na kundi linalo jiita dola la Kiislam IS.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imetoa waranti wa kukamatwa kwa rais wa Sudan Omar al Bashir kwa mauaji ya kimbari, uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Hata hivyo kiongozi huyo wa Sudan pia alikwenda Jordan mwaka jana kuhudhuria mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa wa nchi za Kiarabu, na wala hakukamatwa pale alipotua mjini Amman.

Mwandishi:Zainab Aziz/APE/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga