1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi kuu la upinzani Syria kuhudhuria mazungumzo ya Geneva

30 Januari 2016

Kundi kuu la upinzani nchini Syria limesema Ijumaa (29.01.2016)kwamba litahudhuria mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Umoja wa Mataifa nchini Uswisi, na kupunguza hofu kwamba litasusia mazungumzo hayo.

https://p.dw.com/p/1Hm7O
Genf Friedensverhandlungen zu Krieg in Syrien - Staffan de Mistura
Mjumbe maalum wa UN katika Syria De Mistura(kushoto)akikutana na wawakilishi wa SyriaPicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Kamati ya juu ya majadiliano (HNC) kundi linaloungwa mkono na Saudi Arabia limesema "litashiriki katika hatua za amani ili kujaribu kuona nia thabiti ya upande mwingine kwa kupitia majadiliano na kikosi cha Umoja wa Mataifa," baada ya siku nne za sintofahamu kuhusiana na iwapo kundi hilo litajiunga na mazungumzo hayo.

Licha ya mbinyo kutoka mataifa ya magharibi ili kuhudhuria, kundi hilo la HNC hapo kabla lilisema litashiriki katika mazungumzo hayo ya Geneva bila ya makubaliano kuhusiana na misaada kuwafikia mamia kwa maelfu ya watu waliokwama katika miji iliyozingirwa.

Genf Friedensverhandlungen zu Krieg in Syrien - Protest
Maandamano mjini Geneva dhidi ya utawala wa Syria kabla ya mkutano kuanzaPicha: Reuters/D. Balibouse

Mjumbe mwandamizi wa HNC ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kamati hiyo itatuma "kiasi ya watu 30, hadi 35" katika mazungumzo hayo, ambayo yalianza rasmi jana Ijumaa (29.01.2016)katika msukumo mkubwa kabisa wa kisiasa ambao haujawahi kuwapo ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria ambavyo vimedumu kwa miaka mitano sasa.

Katika ujumbe uliotolewa katika ukurasa wa Twitter, hata hivyo kundi la HNC limesisitiza kwamba litakuwa huko " kushiriki katika mazungumzo na Umoja wa Mataifa na sio majadiliano".

Majadiliano yaanza

Yakiungwa mkono na mataifa ya nje yanayohusika katika vita nchini Syria, mazungumzo hayo yanalenga katika kumaliza mzozo huo ambao umesababisha zaidi ya watu 260,000 kuuwawa na kuchochea kupata nguvu kwa kundi la Waislamu wenye itikadi kali la Dola la Kiislamu.

Waziri wac mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry , Ufaransa na Saudi Arabia, ambako kundi la HNC lina makao yake, wamekaribisha uamuzi huo wa dakika za mwisho wa kundi hilo kutuma wajumbe.

Wawakilishi kutoka serikali ya rais wa Syria Bashar al-Assad waliwasili mapema jana Ijumaa kwa mkutano wao wa kwanza na mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa Staffan de Mistura.

Ujumbe huo wenye watu 16 ulikutana na mpatanishi wa Umoja wa mataifa kwa muda wa masaa matatu, na kuondoka katika jengo la makao makuu ya Umoja wa mataifa bila ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Genf Friedensverhandlungen zu Krieg in Syrien - Medien
Waandishi wa habari wakiweka vyombo vyao tayari kabla mkutano kuanza mjini GenevaPicha: picture-alliance/dpa/M. Trezzini

De Mistura amesema mazungumzo yake ya awali na HNC yanaweza kuwa ama mapema leo ama kesho Jumapili, akiwaambia waandishi habari "watakuwa na kazi ... bila shaka itakapofika Jumatatu".

Ufafanuzi kuhusu mazungumzo

Kundi la HNC hapo kabla lilidai kusitishwa kwa mashambulizi ya mabomu dhidi ya raia, pamoja na makubaliano kuhusu misaada ya kiutu ili kupunguza mateso yanayowapata raia katika miji iliyozingirwa, kabla ya kukubaki kushiriki katika mazungumzo hayo.

Na kundi hilo limeomba "ufafanuzi" baada ya Umoja wa Mataifa kuwaalika wajumbe wengine wa upinzani ambao wanafikiriwa kuwa na mahusiano ya karibu na Urusi na ushawishi mdogo katika mapambano ndani ya nchi hiyo.

Genf Friedensverhandlungen zu Krieg in Syrien - Protest
Wanaharakati wakiandamana kuhusu Syria mjini GenevaPicha: Reuters/D. Balibouse

Kundi la HNC na waungaji mkono wake Saudi Arabia na Uturuki pia limepinga kushiriki kwa makundi ya Wakurdi wa Syria ambao wamepata mafanikio makubwa dhidi ya kundi la Waislamu wenye itikadi kali la Dola la Kiislamu kaskazini mwa Syria katika miezi ya hivi karibuni.

Flüchtlinge Grenze Mazedonien Serbien Balkan Route Winter Kälte
Wakimbizi kutoka Syria wakiwa katika mpaka wa Serbia wakati huu wa baridi kaliPicha: Reuters/M.Djurica

Asaad al-Zoabi , kiongozi wa ujumbe wa HNC, amekituo cha televisheni cha Sky News Arabia kwamba kundi hilo limepata uhakikisho inaoutaka kutoka Marekani na Saudi Arabia, na kuongeza kwamba ujumbe huo utawasili jioni ya Jumamosi ama Jumapili asubihi.

HNC haikutangaza ni nani atatumwa mjini Geneva , lakini limesema hapo kabla kwamba ujumbe wa hapo baadaye utajumuisha wanawake na wajumbe wa makundi ya wachache ya kidini.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: