1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la Alshabaab lajiimarisha tena?

28 Oktoba 2016

Kundi la Al-Shabab limeidhibiti miji 4 ambayo iliachiliwa na wanajeshi wa Ethiopia walioondoka. Hali hiyo inawatia hofu maafisa nchini Somalia, ikizingatiwa uchaguzi wa urais nchini humo unatarajiwa baadaye mwezi Novemba

https://p.dw.com/p/2Rnis
Somalia al-Shabaab Kämpfer
Picha: picture alliance/AP Photo/M. Sheikh Nor

Kundi la kigaidi la al Shabab linaonekana kuinuka tena baada ya kuiteka miji 4 nchini Somalia kando na kufanya shambulio katika nyumba ya kulala wageni mjini Mandera-Kenya na kuua watu 12.

Kuibuka upya kwa kundi hilo lenye uhusiano na mtandao wa al Qaeda, kunaweza kuathiri mipango ya Somalia kuandaa uchaguzi wake mkuu mwezi ujao, na kuyumbisha taifa hilo ambalo ni miongoni mwa mataifa ambayo yameshindwa kujiendeleza kabisa.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kundi hilo lilipoteza udhibiti wa ngome zake kuu ikiwemo jiji kuu la Somalia Mogadishu mnamo mwaka 2011. Hiyo ni kutokana na operesheni inayofanywa dhidi yao na wanajeshi elfu 22,000 wa Umoja wa Afrika - AMISOM hasa kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Ethiopia na  Djibouti. Jeshi dhaifu la Somalia lenye askari wapatao 35,000 pia imeshiriki katika vita dhidi ya al-Shabab.

Kundi la al-Shabab lilikuwa linadhibiti tu vijiji na maeneo kame ya Somalia, ambako pia lilifanyia mipango ya kufanya mashambulio ya kujitoa muhanga jijini Mogadishu na kwenye vituo vingine.

Katika miezi ya hivi karibu, kumekuwa na ongezeko la mashambulizi  dhidi ya hoteli. Kundi hilo pia limeshambulia moja kwa moja kambi za majeshi ya Umoja wa Afrika nchini Somalia.

Wanajeshi wa Somalia katika eneo la shambulio mjini Mogadishu
Wanajeshi wa Somalia katika eneo la shambulio mjini MogadishuPicha: picture-alliance/dpa/S. Y. Warsame

Lakini mwezi huu, Ethiopia iliyokuwa na wanajeshi 2,000 chini ya AMISOM na idadi isiyojulikana iliyoendesha shughuli zake binafsi, iliwaondoa wanajeshi wake katika miji ya Halgan, El-Ali na Mahas katika eneo la Hiran kusini mashariki mwa Somalia.

Bila kuchelewa, baada ya saa chache wapiganaji wa al-Shabab wakadhibiti miji hiyo na kupandisha bendera yao nyeusi.

Siku ya Jumatano, wanajeshi wa Ethiopia walijiondoa katika miji 4, Tiyeglow, kusini magharibi mwa eneo la Bakool, na al-Shabab ikalidhibiti.

Hatua hizo za haraka za al-Shabab kudhibiti miji ambayo imeachiliwa, imewatia hofu maafisa nchini Somalia, hasa ikizingatiwa uchaguzi wa urais nchini humo unatarajiwa baadaye mwezi Novemba.

Haijajulikana ni idadi gani ya wanajeshi wa Ethiopia wameondolewa nchini Somalia. Lakini wadadisi wanasema waliondolewa kutokana na haja ya Ethiopia kudumisha usalama ndani ya nchi yake ili kuimarisha amri ya hali ya hatari iliyotolewa na serikali kwa lengo la kutuliza maandamano dhidi ya serikali ambayo yamedumu kwa miezi kadhaa sasa.

Mchambuzi wa kisiasa nchini Somalia Mohamed Sheikh Abdi amesema, kurudi kwa wanajeshi wa Ethiopia kuliacha pengo lisiloepukika.

Wakati huohuo raia nchini Somalia wanakabiliwa na hatari ya maisha kufuatia kuondoka kwa wanajeshi hao. Wakaazi wa maeneo ambayo al-Shabab imedhibiti tena, wameliambia shirika la habari la Associated Press kwa njia ya simu kuwa kundi hilo linawaua baadhi ya watu wanaoshukiwa kuwa washirika wa karibu wa serikali. Bila kutaka majina yao kutambuliwa, wamesema " ni heri kuwa na Alshabaab hapa kuliko kuwa na wanajeshi wasiotabirika na kutuacha hatarini”.

Vikosi vya usalama vya Somalia katika eneo la mlipuko wa bomu
Vikosi vya usalama vya Somalia katika eneo la mlipuko wa bomuPicha: Reuters/F. Omar

 Msemaji wa serikali ya Ethiopia Getachew Reda amesema, kuondolewa kwa wanajeshi kutoka maeneo mengine hakukuhusisha mipango ya kuachia jeshi la Somalia udhibiti wa maeneo hayo. "Lakini si lazima kwa wanajeshi tunaowatuma Somalia kivyetu, kukaa humo jinsi wale wanaohudumu chini ya Umoja wa Afrika wanavyofanya.” Getachew ameongeza.

Hata hivyo amesema wanajeshi walioondolewa Halagan walipelekwa katika kambi ya nyinginezo, na hivyo kuondolewa kwa wanajeshi hao hakuhusiani kivyovyote na hali ya hatari iliyotangazwa tarehe 8 mwezi huu nchini mwake kufuatia  fujo ambazo zimedumu kwa miezi  6.

Aliisihi jamii ya kimataifa kuingilia kati na ichukue hatamu kutoka kwao sasa, kwani kusalia kwa vikosi vyao ndani ya Somalia kwa muda usiojulikana mwisho wake, kutakuwa hali ya juu ya kutowajibika.

Somalia na maafisa wengine wa Muungano wa Afrika hawakuwepo kuzungumzia suala hilo la kujiondoa kwa wanajeshi mwezi huu. Majeshi ya Somalia yanapaswa kuwajibika zaidi wakati ambapo vikosi vya Umoja wa Afrika vikijiandaa kuondoka ifikapo mwisho wa mwaka 2020. Lakini mashambulio ya mwezi huu yanaashiria kuwa huenda majeshi ya Somalia hayawezi kushikilia faida zilizoletwa na vikosi vya Muungano wa Afrika ambavyo viliinyima al-Shabab udhibiti wa baadhi ya maeneo mengi.

Kufufuka kwa al-Shabab kunajiri baada ya mgawanyiko wa kundi hilo, huku baadhi yao wakiegemea upande wa kundi la Dola la Kiislamu IS badala ya al-Qaeda. Mrengo unaoegemea kundi la Dola la Kiislamu ulidai kuwa umedhibiti mji mmoja kaskazini mwa eneo linalojisimamia kivyake Puntland. Hata hivyo kwa mujibu wa wakaazi wa mji huo, wapiganaji hao wa al-Shabaab walijiondoa baadaye Jumanne usiku.

Mwandishi: John Juma/APE

Mhariri: Gakuba Daniel

   ___