1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la 'Ndrangheta lalengwa katika uvamizi barani Ulaya

Amina Mjahid
6 Desemba 2018

Polisi nchini Italia imesema imewakamata watu kadhaa wanaoshukiwa kuwa wahalifu barani Ulaya na Amerika ya Kusini katika msako mkubwa wa kimataifa uliofanywa na kulilenga genge la mafia la 'Ndrangheta.

https://p.dw.com/p/39ZA1
Deutschland Razzia gegen italienische Mafia
Picha: picture-alliance/dpa/C. Reichwein

Kulingana na shirika la Umoja wa Ulaya linalohusika na masuala ya kimahakama na kukabiliana na uhalifu wa mipaka ya nchi za Ulaya Eurojust, watu takriban 90 wakiwemo wanachama wakuu wa kundi la mafia linalojulikana kwa ulanguzi wa madawa ya kulevya na utakatishaji wa fedha walikamatwa katika uvamizi uliopangwa katika mataifa takriban sita.

Uvamizi huo ambao haukutegemewa dhidi ya kundi hilo lililoko Calabria, Kusini mwa Italia, umekuja siku moja baada ya polisi nchini humo kumkamata kiongozi wa kundi jingine la Mafia.

Maelfu ya maafisa wa polisi walishiriki uvamizi wa jana Jumatano ambapo tani nne za madawa ya kulevya aina ya Coccaine, kilo 120 ya madawa mengine aina ya Ecstasy na kiasi cha pesa cha euro milioni mbili zilikamatwa. Uvamizi huo ulifanyika nchini Ujerumani Uholanzi, Ubelgiji, Luxembourg, Italia  na Suriname.

Genge la mafia la Ndrangheta laonywa kuwa sheria na mahakama za ulaya bado zinafanya kazi

Deutschland Razzia gegen italienische Mafia
Maafisa wa polisi Ujerumani wakiwa katika harakati za operesheni zao dhidi ya kundi la mafia la NdranghetaPicha: picture-alliance/dpa/C. Reichwein

Kwa upande wake Filippo Spiezia Naibu rais wa mahakama ya Umoja wa Ulaya amesema hatua ya uvamizi ni ya kutuma ujumbe kwa wahalifu barani Ulaya kuwa mahakama na sheria za Ulaya zinafanya kazi. Filipo pia amesifu juhudi za mataifa kuungana na kupambana na kundi hilo la Uhalifu.

Kwa ujumla watu 41 walikamatwa nchini Italia, 21 Ujerumani, watu 14 Ubelgiji huku watu watano wakikamatwa uholanzi na wengine wawili nchini Luxembourg. Eurojust  imesema bado inaendelea na operesheni yake ya kuwakamata walahlifu wa kundi hilo la mafia la 'Ndrangheta, huku Polisi nchini Italia ikisema hii ni hatua ya mwanzo tu ya kuzifikisha mwisho  shughuli za kundi hilo duniani kote.

Wakati huo huo polisi ya shirikisho la Ujerumani imesema uvamizi mkali uliofanyika hapo jana ulielekezwa hasa katika jimbo la Magharibi la North Rhine-Westphalia, linalopakana na Uholanzi na Ubelgiji pamoja na jimbo la Bavaria katika eneo la Kusini mwa Ujerumani kunakoaminika kuzidi kusambaa kwa mtandao wa kundi hilo la mafia la 'Ndrangheta.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/dpa/AP

Mhariri: Yusuf Saumu