1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la mashauriano lajadili hali nchini Guinee

Oumilkher Hamidou13 Oktoba 2009

Rais Yar'Adua wa Nigeria aitisha mkutano wa viongozi wa ECOWAS mjini Abuja

https://p.dw.com/p/K56M
Kiongozi wa kijeshi wa Guinee Dadis CamaraPicha: DPA

Jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika Magharibi-ECOWAS imesema viongozi wake watakutana wiki hii kutathmini namna ya kuipatia ufumbuzi migogoro ya Guinee na Niger ambayo rais wa Nigeria anahofia isije ikaenea katika eneo zima.

Rais Umaru Yar'Adua wa Nigeria ametoa mwito mkutano wa kilele wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika Magharibi-ECOWAS ufanyike jumamosi ijayo mjini Abuja kujadili mada hizo mbili,yaani migogoro ya Guinee na Niger.

"Yaliyofanywa na wakuu wa kijeshi wa Guinee ni kinyume na makubaliano yote yaliyowahi kufikiwa na ndugu yangu wa Niger anaendelea kupitisha hatua zinazotoa ishara mbaya kote ulimwenguni-" amesema rais Yar'Adua ambae ndie mwenyekiti wa sasa wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika magharibi-ECOWAS.

Hapo rais Yar'Adua alikua akizungumzia uamuzi wa rais Mamadou Tandja wa Niger wa kubadilisha katiba ili kumuezesha asalie kwa mhula wa tatu madarakani,baada ya kulivunja bunge na mahakama kuu zilizokua zikipinga mipango yake.

"Tumemwaga damu nyingi na hasara kubwa imepatikana katika mapambano ya kupigania demokrasia,kwa hivyo hatuwezi kujiruhusu kuanzisha migogoro mengine."Amesisitiza kiongozi huyo wa Nigeria.

Mkutano wa kilele wa Ecowas utazungumzia mapandekezo

yaliyotolewa na kundi la mashauriano la kimataifa lililokutana jana mjini Abuja.

Mbali na mkutano huo wa kundi la mashauriano,baraza la amani na usalama la umoja wa Afrika linatazamiwa pia kukutana kujadili migogoro hiyo,kama naibu katibu mkuu wa kundi la kimataifa la mashauri kuhusu Guinee,Prof.Ibrahima Fall alivyosema wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kundi hilo mjini Abuja:

"Tunakutana hapa kabla ya ya mkutano wa baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika kwa daraja ya mabalozi wiki ijayo,na baadae mkutano wa kilele wa viongozi wa taifa.Kwa hivyo tunakutana katika wakati ambapo hali ni ngumu na tete kuhusiana na mada zilizotuleta pamoja."

Ikiwa nchi hizo mbili,Niger na Guinee hazitofuata mapendekezo yaliyopitishwa,kuna hatari ya kupitishiwa vikwazo-Amesema Bagudu Hirse,waziri wa dola katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya Nigeria.

Kundi la Mashauriano la kimataifa,linalowajumuisha pia wawakilishi wa Umoja wa ulaya,Umoja wa mataifa na umoja wa Afrika limetoa mwito waandamanaji wote wanaoshikiliwa Guinee waachiwe huru na uhuru wa watu kukusanyika na kutoa maoni yao uheshimiwe.

Kundi hilo limemtaka pia kiongozi wa kijeshji wa Guinee Moussa Dadis Camara athibitishe kua si yeye na wala si mwanajeshi yeyote,hakuna atakaepigania kiti cha rais uchaguzi utakapoitishwa january mwakani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir (AFP&Reuters)

Mhariri:Abdul-Rahman