1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kundi la Taliban lamuandikia Malala barua

MjahidA18 Julai 2013

Kamanda wa ngazi ya juu wa kundi la Taliban nchini Pakistan amemuandikia barua Malala Yousafzai, mwanaharakati kijana mdogo nchini Pakistan akimshutumu kwa kulipaka matope kundi hilo na kumtaka arudi nyumbani.

https://p.dw.com/p/19A8m
Malala Yousafzai
Malala YousafzaiPicha: Reuters

Wapiganaji hao kutoka kundi la Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP) walimpiga Malala risasi kichwani katika kijiji chake cha Swat mwezi Oktoba mwaka jana wakati alipokuwa anapigania haki ya kwenda shule kwa watoto wa kike.

Katika Barua hiyo iliopatikana, Adnan Rasheed mwanachama wa zamani wa jeshi la anga nchini Pakistan ambaye kwa sasa amejiunga na kundi la TTP amesema anatamani kuwa shambulizi dhidi ya Malala lisingefanyika lakini wakati huo huo akamshutumu kwa kufanya kampeni dhidi ya Taliban.

"Uliposhambuliwa na kundi hili nilishtuka sana, natamani jambo hili lisingefanyika lakini nilikuwa nimekushauri hapo awali,Taliban wanaamini kuwa ulikuwa na nia ya kudidimiza juhudi zao za kuwa na mfumo wa kiislamu katika kijiji cha Swat na maandiko yako yalikuwa ya uchokozi" Alisema Adnan Rasheed.

Waasi wa Taliban
Waasi wa TalibanPicha: picture alliance / Ton Koene

Kamanda huyo wa ngazi ya juu ya kundi la Taliban nchini Pakistan alikanusha kwamba Malala alipigwa risasi kwa sababu ya kutaka elimu na kusema kwamba kushambuliwa kwa mwanaharakati huyo wa elimu kunatokana na propaganda zake kwa kundi hilo.

Inasemekana Malala mwenyewe bado mpaka sasa hajapokea barua hiyo licha ya kufahamu yaliomo ndani ya barua.

Rasheed amemshutumu Malala kwa kuunga mkono mfumo wa elimu ya Uingereza na kusema kwamba wanafunzi wanapaswa kusoma dini ya kiislamu na siyo dini ya kishetani.

Kwa sasa kundi hilo limemtaka Malala kurudi nyumbani na kujiunga na shule ya mafundisho ya dini, yani Madrassa ili kujifunza zaidi dini ya kiislamu.

Hotuba ya kusisimua ya Malala kwa Umoja wa Mataifa

Baada ya kupigwa risasi Malala alitibiwa nchini Uingereza ambako anaishi mpaka sasa akiwa na familia yake.

Malala ambaye mwezi huu alitimiza miaka 16 alitoa hotuba ya kusisimua kwa Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza tangu aliposhambuliwa na kundi la Taliban. Malala aliapa kuendelea na masomo yake na kutokubali kunyamazishwa na kundi hilo.

"Tarehe 9 mwezi wa Oktoba mwaka wa 2012, wataliban walinipiga risasi kichwani, na wakawapiga risasi wenzangu pia, walidhani risasi zingetunyamazisha lakini walishindwa" Alisema Malala Yousafzai.

Malala Yousafzai akitoa hotuba yake kwa Umoja wa Mataifa
Malala Yousafzai akitoa hotuba yake kwa Umoja wa MataifaPicha: picture-alliance/dpa

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Gordon Brown ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa katika maswala ya elimu, na aliyekuwa na Malala tangu alipopigwa risasi ameijibu barua hiyo akisema hakuna mtu yoyote atakayeamini kile kinachosemwa na Taliban linapokuja suala ziima la elimu ya mtoto wa kike hadi pale watakapowacha kuzichoma moto shule na kuwauwa wanafunzi wanaopigania haki yao ya elimu.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFPAP/Reuters

Mhriri:Mohammed Abdul-Rahman