1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni kufanyika Jumapili nchini Syria

Josephat Charo25 Mei 2007

Barabara za Syria zimejaa mabango ya rais Bashar Al Assad wa nchi hiyo yakiwa na maneno yasemayo ´Tunakupenda´. Kesho kutafanyika kura ya maoni nchini Syria huku rais Assad akijiandaa kugombea awamu ya pili ya madaraka nchini humo.

https://p.dw.com/p/CHDi
Rais wa Syria Bashar al Assad
Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: dpa

Kampeni za uchaguzi zimepamba moto huku mikutano, densi na vyakula vya jioni vikiandaliwa chini ya mahema makubwa. Vyombo vya habari vya serikali vinampigia debe rais Assad aliyechukua madaraka kufuatia kifo cha babake mnamo Juni mwaka wa 2000.

´Tunakupenda´ ni mojawapo ya maneno yaliyochapishwa kwenye mabango yaliyotundikwa kila mahali katika barabara za mji mkuu Damascus na maeneo mbalimbali nchini Syria. Maneno mengine yaliyotumiwa kwenye mabango hayo ni ´Ndio kwa kiongozi kijana, Ndio kwa usalama na Tunasema ndio kwa mioyo yetu yote.´

Matokeo rasmi ya kura ya maoni ya mwisho kufanyika nchini Syria yalionyesha kuwa rais Bashar al Assad alishinda asilimia 97 ya kura kwenye kura ya maoni baada ya kuchukua utawala kutoka kwa marehemu babake kwa awamu ya miaka saba.

Tovuti moja ya upinzani nchini Syria imewashauri Wasyria waigomee kura ya maoni hapo kesho. Kwa nini kujisumbua na kwenda kupiga kura? Ina maana gani? Imeuliza tovuti hiyo na kupendekeza kura ya maoni ifanywe kwenye mtandao huo wa mawasiliano wa ´internet´.

Lakini mkaazi wa mjini Damascus, aliyejitambulisha kwa jina la Said, lakini akakataa kutaja jina la familia yake, amesema atapiga kura ya ndio kwa rais Assad akisema Syria imefaulu kuondokana na mizozo kadhaa wakati wa utawala wake, akidokeza mbinyo wa Marekani kuhusu Irak na Lebanon. Mkaazi huyo amesema usalama na udhabiti ni vitu muhimu na kusisitiza kuwa Syria inataka kujiweka kando na mizozo katika nchi jirani za Irak na Lebanon.

Kila usiku kuna misongamano mikubwa ya magari mjini Damascus huku magari yakishindana kupiga ving´ora na watu wakishindana kupiga kelele za kizalendo.

Wabunge wa Syria walimuidhinisha rais Assad kama mgombea pekee kuliongoza taifa mnamo tarehe 11 mwezi huu na chama tawala cha Baath juzi Jumanne kiliwashauri raia wa Syria wajitokeze kwa wingi kuidhinisha utetezi wake wa kiti cha urais.

Katika utawala wake wa miaka saba rais Assad amekabiliwa na mbinyo mkubwa kufuatia mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri, mnamo mwaka wa 2005. Serikali ya mjini Damascus, iliyogomewa na Marekani, imetajwa kuhusika na mauaji hayo.

Alipoingia madarakani rais Assad aliahidi kuleta uhuru mpya na kuifungua jamii ya Syria kwa ulimwengu. Lakini mifumo aliyoirithi kutoka kwa babake haijabadilika. Mageuzi aliyoyaanzisha rais Assad yaliyojulikana kwa jina ´Damascus Spring´ hayakudumu kwa muda mrefu huku viongozi walioitawala Syria pamoja na babake wakiutatiza mpango wake huo na kumuelekeza katika sera za kidini na kiimla.

Mapema mwezi huu Marekani iliikosoa Syria kwa kuwahukumu vifungo jela watetezi wa kisiasa kama ishara ya tabia ya kukiuka haki za binadamu inayoendelea kufanywa na nchi hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa kura ya maoni hapo kesho inafanyika wakati mafuta ya Syria yakiendelea kupungua na Wasyria asilimia 10 wakiishi katika umaskini huku wakikabiliwa na ukosefu wa makaazi na mfumuko mkubwa wa bei. Ripoti hiyo imesema uchumi wa Syria ulikua kwa asilimia 5.4 mnamo mwaka jana.