1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni Sudan kusini

10 Januari 2011

Maelfu ya Wasudan ya kusini wamejitokeza tena leo katika siku ya pili ya zoezi la upigaji kura ya maoni kuamua iwapo wanataka kujitenga na wenzao wa kaskazini na kuunda taifa lao jipya.

https://p.dw.com/p/zvkA
Mlolongo wa Wasudan ya kusini wakisubiri kupiga kuraPicha: picture alliance/dpa

Huku wakiwa na shangwe kama walizozionesha jana katika siku ya kwanza ya zoezi hilo, Wasudan ya kusini wamejitokeza kwa wingi tena leo katika vituo vya kupigia kura vilivyoko katika mji mkuu wa eneo hilo Juba.

Licha ya viongozi wa Sudan ya kusini kuwahamasisha watu kujitokeza kupiga kura hapo awali, lakini wingi wa watu waliojitokeza hususan jana uliwashtua pia waratibu wa zoezi hilo.

Na licha ya zoezi hilo kupangwa kumalizika saa kumi na moja jioni za Sudan, vituo vingi vya kupigia kura, vilikuwa wazi kwa saa mbili zaidi na hata zaidi ili kuuwezesha umati wa watu waliojitokeza kufanikisha azma yao hiyo ya kupiga kura, kutokana na kujitokeza kwa wingi zaidi ya ilivyotarajiwa.

Kiir aongoza zoezi la kupiga kura

Referendum Südsudan
Rais wa Sudan ya kusini Salva Kiir, baada ya kupiga kuraPicha: AP

Rais wa Sudan ya kusini Salva Kiir alikuwa mmoja ya Wasudan ya kusini wa mwanzo kupiga kura zao mjini Juba jana na kuliita tukio hilo kuwa ni la kihistoria, na kuwataka wale waliokosa nafasi katika siku ya kwanza, kutokata tamaa.

Miongoni mwa watu maarufu walioshuhudia Rais huyo wa Sudan ya kusini akipiga kura yake ni pamoja na Mjumbe maalumu wa Marekani, nchini Sudan Scott Gration, Seneta John Kerry na mchezaji filamu nyota maarufu wa Hollywood George Clooney.

Wingi huo wa watu waliojitokeza katika siku mbili mfululizo kati ya siku saba zilizowekwa kupiga kura hiyo, ni hatua kubwa kuikaribia asilimia 60 ya kuweza kufanikisha makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2005 kati ya upande wa kaskazini na kusini.

Dschuba al-Baschir
Rais wa Sudan, Omar al-BashirPicha: dapd

Kwa upande wake Rais wa Sudan Omar al Bashir amesema ataheshimu matokeo ya kura hiyo iwapo yatakuwa huru na wazi.

Naye Rais Barack Obama wa Marekani amewapongeza Wasudan ya kusini kwa kufanikisha vizuri siku ya kwanza ya zoezi hilo na kuahidi kuunga mkono.

Matokeo kutolewa baada ya mwezi

Matokeo rasmi ya zoezi hilo yanatarajiwa kutolewa mwezi ujao, kutokana na ugumu uliopo wa kukusanya kura hizo kutokana na tatizo la miundombinu, lakini matokeo ya awali yanatarajiwa kuanza kutolewa mwishoni mwa mwezi huu, kama anavyoelezea zaidi Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa ambaye ambaye ameteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon kuongoza jopo la tume ya watu watatu kuangalia mchakato wa kura za maoni Sudan Kusini.

Takriban watu milioni 3.75 walijiandikisha kupiga kura kusini mwa Sudan na wengine 117,000 waliandikisha Sudan ya kusini, na wengi wakiwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum. na zoezi hilo pia limefanyika katika nchi nyingine nane, ambako Wasudan ya kusini wanaishi.

Referendum Südsudan
Wanawake pia walijitokeza kwa wingiPicha: AP

Kura hiyo ya maoni ni moja ya makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2005 kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe katik ya Sudan ya Kusini na kaskazini vilivyosababisha vifo vya takriban watu milioni mbili na wengine milioni nne kuyakimbia makaazi yao.

Wakati zoezi hilo likiendelea imeripotiwa leo kwamba watu 23 wameuawa katika mapigano na jamii ya wafugaji wa kiarabu katika mpaka wa Sudan ya kusini na kaskazini.

Mwandishi: Halima Nyanza (afp, Reuters)
Mhariri: Josephat Charo