1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura ya maoni Sudan ya Kusini hii hapa

Admin.WagnerD7 Januari 2011

Wanadiplomasia wa mataifa ya Magharibi, viongozi wakongwe na hata wasanii maarufu wa Hollywood wameshawasili kwenye eneo la Kusini ya Sudan wakati wakaazi wanajiandaa kwa kura ya maoni itakayoiamua hatma ya eneo lao.

https://p.dw.com/p/zush
Rais wa Sudan, Omar al_bashir akiwapungia mkono wananchi wakati wa ziara yake Kusini mwa Sudan
Rais wa Sudan, Omar al_bashir akiwapungia mkono wananchi wakati wa ziara yake Kusini mwa SudanPicha: AP

Viongozi hao walifanya mazungumzo ya mwisho mwisho na waandaaji wa kura hiyo ya maoni yaliyokuwa na azma ya kuviondoa vikwazo vya aina yoyote il,e kabla ya siku ya siku. Eneo la Kusini mwa Sudan limesubiri kiasi ya miaka 50 kabla ya kuitimiza hatma yake ya kutaka kujitenga.

Hivi sasa shamra shamra zinaendelea katika eneo la zima la Kusini, huku zoezi la kupiga kura litakaloanza Jumapili ijayo likitarajiwa kuchukua muda wa wiki nzima.

Akizungumza na wakazi wa Juba waliokusanyika, Rais wa zamani wa Afrika Kusini,Thabo Mbeki, anayeuongoza ujumbe wa Umoja wa Afrika uliosimamia mazungumzo kati ya serikali na kusini na kaskazini mwa Sudan alisema kuwa zoezi hilo lina azma ya kuwapa uhuru wakazi wa eneo la Kusini mwa Sudan

Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, na Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa wa zamani, Kofi Annan, wako nchini Sudan ili kulishuhudia zoezi hilo la kihistoria.Wakati huohuo Shirika la Umoja wa mataifa la wakimbizi, UNHCR, limetoa taarifa inayoeleza kuwa kiasi ya Wasudan Kusini 120,000 wamerejea wakitokea Kaskazini ili waweze kushiriki katika zoezi hilo. Wengi wao wanaripotiwa kurejea kwa kuhofia usalama endapo Sudan ya Kusini itajitenga na kuwa taifa huru. Rais wa Afrika kusini wa zamani Thabo Mbeki naye pia aliligusia hilo

Hii leo mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya inayohusika na masuala ya haki za binadamu, Navi Pillay, aliutolea wito uongozi wa Sudan kuhakikisha kuwa vitendo vya unyanyasaji na mateso vinaepukwa wakati wa zoezi hilo muhimu.

Kura hiyo ya maoni ni sehemu muhimu ya makubaliano ya amani yaliofikiwa mwaka 2005 yaliovimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu zaidi ya miongo miwili.

Mwandishi: Mwadzaya Thelma-RTRE/AFPE

Mhariri: Miraji Othman