1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kura zaendelea kuhesabiwa C.A.R

Admin.WagnerD31 Desemba 2015

Zoezi la kuhesabu kura linaendela katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kufuatia uchaguzi wa rais na wabunge uliyofanyika siku ya Jumatano, katika taifa hilo lililotumbuia katika mzozo mkubwa wa kisiasa na kidini.

https://p.dw.com/p/1HWSm
Afrika Wahlen in Zentralafrika
Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Waangalizi waliripoti kasoro chache baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura katika uchaguzi huo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambao ulicheleweshwa mara kadhaa, kutokana na machafuko na kasoro, huku baadhi ya watu wakitilia mashaka juu ya uwezekano wa makundi ya wanamgambo wanaohusika hasa na machafuko hayo kukubali matokeo iwapo yatakuwa kinyume na matarajio yao.

Wagombea thelathin wanawania nafasi ya rais, katika hatua kubwa ya kuirejsha nchi hiyo kwenye mkondo wa demokrasia, huku viti vyote vya ubunge vikigombaniwa. Mapema misururu mirefu ilishuhudiwa katika vituo vya kupigia kura katika mji mkuu Bangui na katika eneo linalokaliwa na Waislamu wengi la PK5.

Mpigakura akitekeleza wajibu wake.
Mpigakura akitekeleza wajibu wake.Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

"Upigaji kura ulienda vizuri, ukiacha jaribio moja la udanganyifu lililotokea mchana, wakati mtu mmoja alipojaribu kupiga kura kwa kutumia kitambulicho kilichoandikwa jina la mwanamke wakati yeye ni mwanaume," alisema Bienvenu Donatien, msimamizi wa kituo cha kupigia kura mjini Bangui.

Uchaguzi wa bunge kurudiwa baadhi ya maeneo

Karibu watu milioni moja kati ya jumla ya raia milioni tano wa taifa hilo wameyapiga kisogo makaazi yao kutokana na mapigano na kampeni za mauaji ya kidini na kikabila. Tume ya uchaguzi ilisema itarejea uchaguzi wa bunge katika baadhi ya maeneo kwa sababu karatasi za kupigia kura hazikuweza kufika katika maeneo hayo. Lakini hakuna tarehe iliyopangwa kwa ajili ya uchaguzi huo wa marudio.

Timu ya uangalizi kutoka Umoja wa Afrika, ilisema moja ya mambo waliogundua ni sababu ya kucheleweshwa kwa upigaji kura, ambapo kiongozi wa timu hiyo Abdon Ledanganzoui, alisema moja wa wagombea ubunge alisahaulika katika karatasi ya uchaguzi, jambo lililosababisha ucheleweshaji.

"Tulibaini pia kuwa baadhi ya wapigakura walikuwa na vitambulisho vyao vya kupigia kura lakini majina yao hayakuwepo kwenye orodha, lakini mbali na hayo hakukuwa na matatizo makubwa," alisema Ledanganzoui.

Moja wa wagombea urais Anicet Clement Guiyma.
Moja wa wagombea urais Anicet Clement Guiyma.Picha: DW/J. M. Barès

Waasi wa kundi la Seleka, ambao wengi wao ni Waislamu kutoka eneo la Kaskazini waliotelekezwa na serikali zilizopita, walitwaa madaraka mapema mwaka 2013, na kusababisha ulipizaji kisasi kutoka kwa wanamgambo wa kundi la anti-balaka, na tangu wakati huo, viongozi wa makundi hayo wamekuwa wakichochea mauaji ya kidini na kikabila.

Matokeo kamili Januari

Wagombea wanaopewa nafasi kubwa katika uchaguzi huo ni pamoja na mawaziri wakuu wa zamani Anicet - Georges Dologuele na Martin Ziguele, ambaye alipata uungwaji mkono siku ya Jumanne, baada ya wanamgambo wa anti-balaka waliounda chama cha Umoja na Maendeleo cha Jamhuri ya Afrika ya Kati, kusema wanamuunga mkono.

Matokeo ya mwanzo yatatangazwa katika siku zijazo, na mahakama ya katiba laazima itoe matokeo ya mwisho siku 15 baada ya siku ilipopigwa kura.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,rtrtv

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman