1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kuripoti ukweli kunaweza kukusababishia kifo nchini Pakistan.

Mohamed Dahman4 Desemba 2006

Mwandishi wa habari wa mwisho kurepoti kutoka jimbo la Kusini la Waziristan mojawapo ya majimbo ya kikabila yenye vurugu nchini Pakistan linalopakana na Afghanistan ameondoka katika jimbo hilo.Dilawar Wazir Khan mwenye umri wa miaka 38 amesema ametekwa nyara na kuteswa kwa sababu tu ya kurepoti ukweli. Wenzake wengi wameacha kazi hiyo ya uandishi wa habari na wameondoka katika eneo hilo.

https://p.dw.com/p/CHm1
Waziristan jimbo la hatari waandishi wa habari kurepoti nchini Pakistan.
Waziristan jimbo la hatari waandishi wa habari kurepoti nchini Pakistan.Picha: dpa

Dilawar Khan anafanya kazi na Idhaa ya lugha ya Kiurdu ya Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC nchini Pakistan na gazeti la Kingereza la Pakistan litolewalo kila siku la Dawn lenye kumaanisha Kumekucha.

Baada ya kunusurika kuuwawa mara mbili Dilawar Khan amekuja kuandamwa tena na kile waandishi wanachosema kuwa ni kazi ya mashushu wa shirika la ujasusi la Pakistan lenye kuvuma kwa ubaya ISI.Mapema mwezi uliopita Mahkama Kuu nchini Pakistan ilikaripia serikali kwa kutojali haki za binaadamu baada ya familia ya watu 41 kutoweka na kutojulikana ilipo.

Baada ya jaribio la kumuuwa Dilawar Khan kupelekea kuuwawa kwa wenzake wawili Allah Noor Wazir na Amir Nawab na kaka yake mwenye umri wa miaka 15 kutekwa nyara na kuuwawa hapo mwaka 2005 Khan ameona kuwa ni busara kuhama kutoka mji alikozaliwa wa Wana kwenye jimbo la Waziristan Kusini na kwenda kuishi kwenye jimbo la mpaka wa Kaskazini Mashariki.

Amekaririwa akisema kwamba hajuwi pa kwenda kutafuta hifadhi kwamba anaona hakuna mahala penye usalama wa kutosha. Anajiona ana bahati kwa kunusrika safari hii lakini hana hakika iwapo atakuwa na bahati hiyo tena mara nyengine.

Lakini wakati huo huo anakataa kuweka kalamu yake chini. Anasema na kwamba ataendelea kuandika na kurepoti kutokea hapo na kuwa haandiki dhidi ya jeshi au wanamgambo huwa tu anaripoti juu ya kile kinachotokea na kutowa maoni ya pande zote mbili.

Akiwa amezibwa macho na kutiwa pingu mwandishi huyo ameteswa kwa masaa 30 kabla ya kuachiliwa huru.Yumkini ikawa ameokoka kutokana na wito wa kulaani kutekwa kwake wa vyama vya waandishi wa habari pamoja na wito wa kususiwa kwa vikao vya bunge.Mashirika ya habari ya kimataifa pia yaliingilia kati.Matangazo ya lugha ya Kiurdu ya Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC yalitangaza habari za kutekwa nyara kwake kwa siku mbili mfululizo na mkurugenzi wa World Service wa shirika hilo Nigel Capman alitaka seriali ya Pakistan kubainisha mahali alipo mwandishi huyo.

Katika taarifa kufuatia kuachiliwa kwa mwandishi huyo hapo Novemba 21 Joel Simon mkurugenzi mtendaji wa Kamati ya Kuwalinda Waandishi wa Habari yenye makao yake makuu mjini New York amesema shutuma za umma kutokana na kutoweka kwa Dilawar Khan hazipaswi kumalizika hivi sasa kwa kuwa ameachiliwa huru.Kutoweka na vifo vya waandishi habari kadhaa wa Pakistan kumepita bila ya kufafanuliwa,kuchunguzwa na bila ya kurepotiwa na serikali.Polisi na mahkama lazima ziwafikishe mbele ya sheria wale wanaowadhuru na kuwatisha waandishi wa habari.

Juu ya kwamba ameachiliwa huru Dilawar amegoma kufafanuwa habari zozote kuhusu nani waliomteka nyara au kile walichomfanyia.

Hamid Mir mwandishi makala wa lugha ya Kiurdu mtangazaji mashuhuri wa kipindi cha televisheni juu ya masuala ya kisiasa na kijamii nchini Pakistan anasema Dilawar ametekwa nyara kwa sababu ya habari zake kwenye gazeti la Dawn juu ya makubaliano ya amani huko Waziristan Kaskazini kuthibitika kwamba yamesainiwa na wanamgambo na sio na viongozi wa kikabila wa eneo hilo.Aliachiliwa huru kwa sababu gazeti hilo lilichapisha nambari ya gari linalomilikiwa na Shirika la Ujasusi la Pakistan ISI ambalo ndilo lililomchukuwa.

Akifuatilia historia ya kutekwa nyara kwa waandishi habari Mazhar Abbas katibu wa Shirikisho la Vyama vya Waandishi wa Habari nchini Pakistan anasema kulianzia miaka ya1990 ambapo mwandishi mwandamizi alieko Islamabad Hayun Fahr alitiwa ndani na ISI kwa madai ya kufanya kazi dhidi ya maslahi ya taifa. Mwandishi huyo alihukumiwa kifo na mahkama ya kijeshi lakini aliachiliwa huru kutokana na afya kuwa mbaya na alifariki muda mfupi baade.

Abbas anasema wakati kutiwa ndani kusiko halali kwa waandishi kunatokea duniani kote wale wanaoripoti habari za hatari wako hatarini zaidi na wimbi hili la karibuni kabisa ni zawadi ya vita vya ugaidi.