1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Historia

Kutana na Cheikh Diop, mwanasayansi wa Kiafrika

Mohammed Khelef
25 Julai 2018

Msomi huyu wa Kisenegali anatajwa kuwa baba wa mtazamo wa Kiafrika katika uchambuzi wa historia ya dunia. Ndiye aliyeanzisha hoja ya kuwa watawala wa zamani wa Misri, Mafirauni, hawakuwa watu weupe, bali Waafrika weusi.

https://p.dw.com/p/2tMRo

Cheikh Anta Diop aliishi wakati gani? Cheikh Anta Diop alizaliwa mwaka 1923 katika kijiji cha Thieytu, takriban kilomita mia moja magharibi mwa Dakar, nchini Senegal, katika familia ya Wolof yenye asili ya mabwenyenye. Alipata udhamini wa kusomea Ufaransa mwaka 1946. Alichagua fizikia na Kemia kabla ya kubadilisha kufanya filosofia na historia akaandika tasnifu iliyoangazia ``Afrika ya Watu Weusi kabla ya Mkoloni.`` na `` Umoja wa utamaduni wa Mwafrika Mweusi.`` Cheikh Anta Diop alikuwa mzalendo na mtetezi wa shirikisho la Afrika. Alirejea Senegal mwaka 1960 wakati  taifa hilo lililopojinyakulia uhuru na akajitwika majukumu ya kufunza, kutafiti na siasa hadi alipofariki dunia mwaka 1986.

African Roots Cheikh Anta Diop
Picha: Comic Republic

Je, Cheikh Anta Diop alifahamika kwa kitu gani?

Cheikh Anta Diop alikuwa mwandishi aliyebobea: Ndiye mwadishi wa kazi nyingi za sayansi na vitabu kuhusu historia ya bara la Afrika, lakini pia kuhusu mustakabali wake.

  • Akizingatia nadharia ya undugu kati ya lugha za Kiafrika kama vile Wolof- lugha ya kwanza ya mamake-na lugha ya zamani ya Misri, Cheikh Anta Diop alifichua kuwa athari ya utamaduni wa Waafrika wa zamani katika maisha ya Wamisri wa kale na alionesha kuwa "Misri ya kale ilikuwa ya watu weusi."
  • Cheikh Anta Diop alikuwa na shahada katika masomo ya kemia na fizikia ya nyuklia na aliunda maabara ya kwanza ya Kiafrika ya kutambua umri wa viumbe hai mwaka 1966 katika chuo hicho ambacho kimepewa jina lake. 
  • Nyakati alipokuwa mwanafunzi, alikuwa mtetezi wa uhuru wa mataifa ya Afrika. Baadaye alikuja akawa mhimili muhimu katika  vuguvugu la Shirikisho la Afrika na akawasilisha mawazo yake kwa mhariri wa jarida la  masuala ya uchumi na utamaduni la shirikisho la dola la waafrika (1960, editor: présence africaine).

Je, unaweza kunipa baadhi ya nukuu za Cheikh Anta Diop? 

"Misri ni muhimu kwa Afrika nzima ya Weusi kama zilivyokuwa  Ugiriki na Roma barani  Ulaya."

"Wingi wa tamaduni unaweza ukafanya watu kuchangia zaidi ustawi wa binadamu na kufikia watu wengine karibu kwa ufahamu."

"Watu wenye itikadi wanaojificha kwa kisingizio cha sayansi lazima watambue kuwa kipindi cha udanganyifu, usomi bandia, bila shaka zimefika mwisho, kwamba ukurasa wa historia ya mahusiano ya watu umefunguliwa."

Asili ya Afrika: Cheikh Anta Diop

Je, kazi za Cheikh Anta Diop zilikuwa na utata?  Wakati kitabu chake, Utamaduni na Mataifa ya Watu Weusi(1954) kilipochapishwa,Cheikh Anta Diop alikabiliwa na masuala mengi katika ulimwengu wa wasomi mbali na kukikosoa kwa misingi kuwa na chuki na ubaguzi wa rangi uliorithiwa kutoka kwa wakoloni.  Baadhi ya wenzake walimshutumu kwa kuwa na mtazamo wa wingi wa nyanja, ambao wakati mwengine ulichanganya, wengine wakisema kuwa kazi zake za sayansi ziliathiriwa pakubwa na harakati zake za siasa. Ni mwaka 1974 wakati wa Kongamano la Kimataifa jijini Cairo, ambapo mtaalamu mmoja wa masuala ya Misri alipongeza nadharia zake. Tangu wakati huo nadharia zake zimekubaliwa kuwa za kweli.  

Tamara Wackernagel, Mamadou Lamine Ba na Philipp Sandner wamechangia kuandika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na wakfu wa Gerda Henkel.


Mwandishi: Tamara Wackernagel,Mamadou Lamine Ba na Phillip Sandner
Tafsiri: Shisia Wasilwa
Mhariri: Saumu Yusuf