1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kutenguliwa Obamacare kwapata pigo

18 Julai 2017

Jaribio jipya la wabunge wa chama cha Republican nchini Marekani kuufanyia mageuzi makubwa muswada wa sheria wa afya unaojulikana kama Obamacare na kuanzisha muswada mpya limepata pigo kubwa.

https://p.dw.com/p/2gik9
Obama Care Obamacare USA medizinische Versorgung
Picha: Getty Images/J.Moore

Hayo yanajiri wakati utawala wa Trump umeliambia bunge la Marekani kwa mara ya pili hapo Jumatatu kwamba Iran inatimiza masharti ya makubaliano ya nyuklia lakini inaweza kukabiliwa na matokeo mabaya iwapo nchi hiyo itavunja mwamko wa makubaliano ya nyuklia.

Tangazo kutoka kwa maseneta Mike Lee wa jimbo la Utah na Jerry Moran wa Kansas limeziwacha juhudi zilizoahidiwa kwa muda mrefu na chama cha Republican katika vurugu.Kiongozi wa wabunge wa kundi la chama hicho bungeni, Mitch McConnell, ametangaza atachukuwa hatua za kurudi nyuma na kujaribu kupitisha muswada wa moja kwa moja wa kutenguwa muswada huo wa afya wa Obama ambao wabunge wa Republican waliuidhinisha wakati Obama alipokuwa bado yuko madarakani na kuwa na uhakika wa kuupigia kura ya turufu kuuzuwiya.

Inaonekana haiwezekani muswada huo kufanikiwa kwa hivi sasa na kuja kuwa sheria hasa na utasababisha taathira mbali mbali ambazo zitawatia hofu maseneta.

Nyundo ya kifo

USA PK Mitch McConnell
Kiongozi wa wabunge wa chama cha Republikan bungeni Mitch McConnell.Picha: picture-alliance/CNP/MediaPunch/R. Sachs

McConell amesema katika taarifa iliyonekana kama kuupiga nyundo ya kifo muswada huo kwamba "Inasikitisha hivi sasa ni dhahir kwamba juhudi za kutenguwa muswada wa Obamacare hazitoweza kufanikiwa" ili wabunge hao wa chama cha Repiblican waweze kuanzisha muswada mpya wa kuchukuwa nafasi ya ule wa Obama.

Trump ambaye masaa machache kabla ya hapo alitabiri kufanikiwa kwa juhudi hizo za McConell kuutenguwa muswada huo na badala yake kuuweka mwengine mpya ametowa wito kupitia mtandao wa Twitter kwamba wabunge wa Republican wanapaswa tu kuutenguwa muswada huo wa Obama ambao hivi sasa umeshindwa kufanya kazi na kuanza kushughulikia mpango wa mpya wa afya, ambao utaanza mwanzo mpya na kwamba wabunge wa chama cha Democrat nao pia wataunga mkono mpango huo.


Na wakati Trump akikabiliwa na pigo hilo, utawala wake hapo jana kwa mara ya pili umeliambia bunge kwamba Iran inatimiza masharti ya makubaliano ya nyuklia na inaweza kuendelea kunufaika na kuondolewa kwa vikwazo, licha ya kusisitiza kwamba serikali ya nchi hiyo itakabiliwa na matokeo mabaya iwapo itashindwa kuzingatia mwamko wa makubaliano hayo.

Rais Trump ambaye alishutumu makubaliano hayo ya mwaka 2015 wakati alipokuwa mgombea wa urais wa Marekani amejipa muda zaidi aidha ayapuuze au ayazingatie. Badala yake maafisa wake waandamizi wamekuwa wakisisitiza wasiwasi wao mkubwa juu ya mienendo ya nyuklia  ya nchi hiyo na kuapa kwamba tabia hii haitoachwa bila ya kuchukuliwa hatua za adhabu.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif akiwa mjini New York hapo Jumatatu kuhudhuria kikao cha Umoja wa Mataifa kuhusu maendeleo amesema bado hakuzungumzia suala la nyuklia na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson.


Mwandidhi: Mohamed Dahman/AP

Mhariri: Mohammed Khelef