1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwa mara nyingine uadui baina ya Marekani na Iran umezuka

8 Mei 2008

Uhasama wa kisiasa miongoni mwa Washia uliozusha mapigano katika maendeo yaliyoathirika kwa mapigano,nchini Iraq, umezusha tena uadui Mkubwa baina ya Marekani na Iran.

https://p.dw.com/p/DwqH
Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad .Picha: AP

Wakiwa tayari kwa mpango wa Kinyuklia wa Iran, Serikali hizo mbili tayari zimeanza kugongana juu ya mapigano yaliyoko Baghdad katika maeneo yaliyoharibika ya washia kwenye mji wa Sadr, mapigano ambayo yameondoa matumaini ya hivi karibuni juu ya mazungumzo na baraza la ulinzi la Iraq.

Mkurugenzi wa kundi la Kimataifa la kukabiliana na mizozo Mashariki ya Kati lenye makao yake makuu mjini Brussels, Joost(Yost) Hiltermann, amenukuliwa akisema kuwa Ikulu, imegawanyika sehemu moja wakipendekeza kuishambulia Iran, na wengine wakitaka kufunguliwe mazungumzo na nchi hiyo.

Amesema mazungumzo juu ya Iraq yanaonekana kama vile hayana maana yoyote kwa sababu hali ya mapigano inaongezeka katika mji wenye machafuko wa Sadr, mjini Baghdad.

Tangu kuzuka kwa mapigano kwenye mji wa Sadr,baina ya wanamgambo na wanajeshi mwezi Machi, Mamia ya watu wameshauawa katika eneo hilo la Washia ambao wengi wao ni wafuasi wa Moqtada al -Sadr.

Wakati Tehran ikiwa imetupiliwa mbali na majeshi ya Marekani, Majeshi ya Marekani yanayashutumu makundi ya Iran kwa kuwapa silaha wapiganaji wa Kishia.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Iraq, Hoshyar Zebari, alisema kuwa kulikuwa na uwezekano mdogo sana kwa kufanyika kwa awamu ya nne ya mazungumzo baina ya Iran na Marekani wakati hali ya wasiwasi inaendelea katika maeneo ya machafuko.

Waziri Zebari, amesema kuwa mapigano baina ya majeshi ya Marekani na Iraq ikiwemo pia wapiganaji wa Sadr yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na hali ya wasiwasi iliyopo baina ya Marekani na Iran.

Kwa upande wake Iran ilisema hakuna haja ya mazungumzo wakati majeshi ya Marekani yamekuwa yakiendelea kuyashambulia makundi ya Washia, wakati huohuo Marekani ikiripoti kuwa hakuna maana pia iwapo Iran itaendelea kupanga mipango ya kuwasaidia wapiganaji wa Kishia.

Mwaka jana, Marekani na Iran zilifanya awwamu ya tatu ya mazungumzo, ingawa pande zote hizo mbili hazina mahusiano yoyote ya Kibalozi tangu kutokea kwa mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979.

Mapigano katika mji wa Sadr yalizuka baada ya Waziri Mkuu wa Iraq Nuri Al-Maliki kuamrisha operesheni ya Kijeshi dhidi ya kile alichokiita makundi ya wahalifu wanaoendesha shughuli zao Kusini mwa mji huo wa bandari na eneo lenye mafuta mengi la Basra.

Bwana Hiltermann, amepinga matamshi hayo yaliyotolewa na Waziri huyo Mkuu akisema kwamba operesheni hiyo ya Kijeshi ilionekana tangu mwanzo kuelekezwa dhidi ya wafuasi wa Sadr kwa lengo la kunufaisha chama chake cha Dawa pamoja na Muungano Mkuu wa Washia, Baraza Kuu la Kiislam.

Aidha Hiltermann ameongeza kusema kwamba mpango huo wa Serikali ya Nuri Al-Maliki dhidi ya jeshi la Mahdi hautafanikiwa na badala yake utasababisha mvurugano mkubwa kwa makundi yote ya Washia.

Hata hivyo Makamanda wa Kijeshi wa Marekani wameendelea kusisitiza kuwa mapigano yao hayalengi jeshi la Mahdi bali kile wanachokiita kundi maalumu la wahalfu.