1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kwaheri Shujaa wa Afrika

Mjahida15 Desemba 2013

Raia wa Afrika ya Kusini na viongozi mbali mbali duniani wametoa heshima zao za mwisho kwa rais wa zamani wa taifa hilo Nelson Mandela, yaliyofanyika leo 15.12.2013 katika kijiji alichokulia cha Qunu.

https://p.dw.com/p/1AZxD
Jukwaa la maombolezo
Jukwaa la maombolezoPicha: Reuters

Maelfu ya wanachama wa chama tawala cha ANC, familia ya Mandela, marafiki, maafisa wa serikali na wageni waheshimiwa walihudhuria mazishi hayo nyumbani kwa Mandela, mashariki mwa mkoa wa Cape.

Mandela amezikwa karibu na wazazi wake na watoto wake watatu.

Naibu rais wa chama cha ANC, Cyril Ramaphosa, aliwaambia waombolezaji kwamba baba wa taifa anapaswa kuzikwa mchana wakati jua linachomoza vyema, hii ikiwa ni kulingana na mila na tamaduni za ukoo wa Xhosa anakotokea Mandela.

Viongozi wa ANC wakilizunguka jeneza la Mandela
Viongozi wa ANC wakilizunguka jeneza la MandelaPicha: Getty Images

Mazishi ya Mandela yamemaliza siku 10 za maombolezo ya shujaa huyo aliyepambana na tawala za kibaguzi aliyefariki tarehe 5 Disemba akiwa na umri wa miaka 95 baada ya kuugua homa ya mapafu kwa muda mrefu.

Mazishi haya yamewaleta pamoja waombolezaji 4,500 ikiwemo familia yake mwenyewe Mandela, viongozi wa Afrika ya Kusini na dunia kwa ujumla.

Maelfu wahudhuria mazishi ya Madiba

Askofu Mstaafu Desmond Tutu, ambaye mwanzoni ilisemekana hakualikwa kwenye mazishi hayo, alikuwepo sambamba na Mwanamfalme Charles wa Uingereza, mwanaharakati wa kutetea haki za binaadamu wa Marekani Jesse Jackson, pamoja na Oprah Winfrey ni miongoni mwa waliohudhuria mazishi hayo.

Wakati jeneza la Mandela lililofinikwa kwa bendera ya Afrika ya Kusini lilipokuwa linatolewa kutoka nyumbani kwake katika kijiji cha Qunu kupelekwa katika eneo lililotengwa kwa mazishi, mizinga 21 ilipigwa hewani kutoa heshima kwa shujaa huyo wa ukombozi.

Mjukuu wa Mandela, Mandla Mandela, na Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini walikuwepo nyuma ya jeneza hilo wakati lilipokuwa linaingizwa ndani ya eneo la kufanyiwa maombi ya mwisho.

Watu waomboleza kifo cha Mandela
Watu waomboleza kifo cha MandelaPicha: Reuters

Nandi Mandela, mjukuu mwengine wa Mzee Mandela aliyetoa hotuba kwa niaba ya watoto, wajukuu na vitukuu wa Madiba, amesema ni wakati wa Afrika ya Kusini kuendelea kuyaenzi yale aliyoyafanya babu yake.

"Tutajifunza yake uliotufundisha katika maisha yetu, kama waafrika kusini huu sio wakati wa kunyosheana vidole bali ni tutapaswa kufanya mambo mema kwa Afrika Kusini," alisema Nandi.

Viongozi watoa heshima zao

Kwa upande wake, Rais Joyce Banda wa Malawi amemuomba rais wa Afrika Kusini Jacob zuma kuhakikisha kuwa raia wa Afrika Kusini wanaendelea kuungana pamoja na kuwa na amani kama alivyotaka Nelson Mandela.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania pia alitoa ujumbe wake wa risala za rambirambi kwa raia wa Afrika ya Kusini.

"Watu wa Tanzania wanataka mujue kwamba hamuko peke yenu tuko nayi katika wakati huu mgumu na watakuwa nanyi hata baada ya kipindi hiki, wanasema huzuni wenu ni wetu na kuondokewa kwenu pia ni kuondokewa kwetu sisi," alisema Kikwete.

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete
Rais wa Tanzania Jakaya KikwetePicha: dapd

Mzee Madiba amemuacha mjane Grace Machel, mtalaka wake Winnie Madikizela-Mandela, watoto watatu wa kike, wajukuu 18 na vitukuu 12.

Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef