1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KYOTO:Bi Merkel atoa wito wa kupunguzwa kwa gesi za viwanda

31 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBU2

Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel anatoa wito kwa nchi ya Uchina na mataifa mengine yanayoinukia kuweka malengo maalum ya kupunguza gesi za viwanda ili kuzuia ongezeko la viwango vya joto ulimwenguni.Bi Merkel anatoa wito wa hatua kupigwa katika vita vya kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya anga alipozuru mji wa kale wa Kyoto ikiwa ni miaka 10 tangu kufikiwa kwa makubaliano ya Kyoto ya kupunguza viwango vya gesi za viwanda.

Kiongozi huyo wa Ujerumani anapendekeza kufikiwa kwa makubaliano ya kupambana na athari za mabadiliko ya hali anga yanayotilia maanani idadi ya watu katika kila nchi.Pendekezo hilo linataraji kuyahusisha kwa karibu mataifa ya India na Uchina.

Kiongozi huyo alikuwa mwandalizi wa mkutano wa kilele wa kundi la G8 uliofanyika mwezi Juni na kuafiki kupunguza viwango vya gesi za viwanda kw anusu ifikapo mwaka 2050.

Kundi la G8 linajumuisha pia Marekani iliyo mtoaji mkubwa wa gesi za viwanda japo inapinga makubaliano ya Kyoto kwani hayashinikizi mataifa yanayoinukia kama India na Uchina kupunguza viwango vyao vya gesi za viwanda.

Mazungumzo mengine yanapangwa kufanyika mwezi Disemba mwaka huu mjini Bali nchini Indonesia ili kuandaa rasimu itakayofuatwa baada ya makubalino ya Kyoto kumaliza muda wake mwaka 2012.