1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lagarde aepuka kushtakiwa

25 Mei 2013

Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa Christine Lagarde Ijumaa (24.05.2013) aepuka kufunguliwa mashtaka mara moja lakini ametajwa kuwa "shahidi msaidizi" baada ya waendesha mashtaka wa Ufaransa kumhoji kwa siku mbili.

https://p.dw.com/p/18dxu
Christine Lagarde Mkuu wa IMF.
Christine Lagarde Mkuu wa IMF.Picha: Reuters

Lagarde alihojiwa kwa jumla ya saa 24 na waendesha mashtaka wa mahakama inayofanya uchunguzi wa kesi za wizara kwenda kinyume na taratibu wakati wa kushughulikia mzozo ambao umepelekea kulipwa kwa euro milioni 400 kwa mfanya biashara mwenye utata Bernard Tapie.Amewaambia waandishi wa habari wakati alipokuwa anatoka katika mahakama hiyo ya Paris Ijumaa usiku "Daraja aliyowekwa kuwa shahidi wa kusaidia haikumshangaza".

Lagarde mwenye umri wa miaka 57 amesema "daima amekuwa akifanya kazi kwa maslahi ya taifa na kwa mujibu wa sheria." Amekuwa akikanusha kwamba hakufanya kosa lolote lile na kwamba maelezo yake yamekuja kufuatia shaka zilizozuka kutokana na maamuzi aliyoyatowa wakati huo.

Wakati Lagarde ameweza kuepuka kuwekwa chini ya uchunguzi rasmi ambapo kwa daraja ya Ufaransa ni karibu sawa na kufunguliwa mashtaka, kuwa"shahidi wa kusaidia" kunamaanisha kwamba bado anaweza kukabiliwa na masuala zaidi na yumkini baadae akafunguliwa mashtaka.

IMF ina imani na Lagarde

Lagarde amesema sasa anapaswa kurudi Washington Marekani na kuripoti kwa bodi ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ambayo kwa mara nyengine tena imeelezea imani iliokuwa nayo kwa kiongozi wake wa kwanza wa kike baada ya kujuwa uamuzi huo wa mahakama.

Mkuu wa IMF Christine Lagarde akiwapungia watu walioko nje ya mahakama Ijumaa (24.05.2013)
Mkuu wa IMF Christine Lagarde akiwapungia watu walioko nje ya mahakama Ijumaa (24.05.2013)Picha: Reuters

Kwa Lagarde ambaye anahesabiwa kuwa miongoni mwa wanawake wenye sauti kubwa kabisa duniani alijipatia heshima wakati akiwa waziri wa kwanza wa fedha mwanamke nchini Ufaransa kwa msimamo wake wa kutotaka upuuzi,usomi na mtindo wake.

Mashtaka ya uhalifu dhidi ya mama huyo ingelikuwa ni karaha kwa IMF baada ya mtangulizi wake Dominique Strauss-Kahn ambaye pia anatokea Ufaransa kujiuzulu kwa idhara hapo mwaka 2011 kufuatia madai ya dhila ya ngono kwa mhudumu wa kike wa hoteli moja mjini New York.

Msemaji wa IMF Gerry Rice amesema katika taarifa kwamba bodi ya utendaji itaarifiwa tena juu ya suala hilo hivi karibuni na kwamba bodi hiyo imekuwa ikiarifiwa mara kadhaa juu ya suala hilo na kila wakati imekuwa ikielezea imani yake kwa uwezo wa mkurugenzi wake huyo mtendaji kutekeleza kazi zake kwa ufanisi.

Mkuu wa zamani wa IMF Dominique Strauss-Kahn.
Mkuu wa zamani wa IMF Dominique Strauss-Kahn.Picha: Reuters

Uchunguzi huo unamhusisha Tapie mwanasiasa wa zamani ambaye aliwahi kufungwa gerezani kwa kupanga matokeo ya mechi wakati alipokuwa rais wa klabu ya soka ya Ufaransa ya Olympique de Marseille.

Waendesha mashtaka wa Mahakama ya Haki ya Jamhuri (CJR) walimtuhumu kupatiwa upendeleo ili aweze kumuunga mkono Rais Nicolas Sarkozy wakati wa uchaguzi wa rais wa mwaka 2007.Walidokeza kwamba Lagarde wakati huo akiwa waziri wa fedha alihusika kwa kiasi fulani na uvunjaji wa taratibu jambo ambalo lingeliweza kupelekea kufunguliwa mashtaka kwa kushiriki katika ulaghai na ubadhirifu wa fedha za umma.

Uchunguzi ulijikita juu ya hatua yake ya mwaka 2007 ya kulitaka jopo la majaji kusuluhisha katika mzozo wa kuuzwa kwa kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas hapo mwaka 1993 kati ya Tapie na Benki ya Mikopo ya Lyonnais iliosambaratika ambayo kwa kiasi fulani ilikuwa na umiliki wa serikali.Tapei aliishutumu benki hiyo kwa kumghilibu kutokana na kushusha thamani ya kampuni ya Adidas wakati wa kuuzwa kwake na kutaka serikali ikiwa mshika dau mkuu katika benki hiyo kumlipa fidia.

Mzozo ulikuwa wa gharama

Hoja zake zilikubaliwa na jopo la usuluhishi lakini wahakiki wamedai kwamba serikali haikupaswa kutumbukizwa kwenye hatari ya kulazimishwa kulipa fidia kwa mtu aliepatikana na hatia ya uhalifu kwani wakati huo alikuwa amefilisika na asingeliweza kuiwasilisha kesi hiyo mahakamani.

Mfanyabiashara tajiri wa Ufaransa Bernard Tapie.
Mfanyabiashara tajiri wa Ufaransa Bernard Tapie.Picha: AP

Lagarde alisema usuluhishi huo ulikuwa ni muhimu kumaliza mzozo huo wenye gharama kubwa na daima amekuwa akikanusha kwamba alichukuwa hatua hiyo kwa kuamuriwa na Sarkozy.

Malipo aliyopokea Tapie yalimwezesha kulipa madeni yake makubwa na kodi ambapo kwa mujibu wa repoti za vyombo vya habari akibakiwa na euro milioni 20 hadi 40 ambazo alizutumia kuanzisha upya biashara.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri: Caro Robi