1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lavrov azuru Oman kuzungumzia vita vya Ukraine

Lilian Mtono
11 Mei 2022

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergey Lavrov amefanya ziara ya kushtukiza nchini Oman na kufanya mazungumzo na maafisa wa nchini humo kuhusiana na vita vinyoendelea nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4B97l
Sergej Lawrow
Picha: Sergei Ilnitsky/POOL/AFP/Getty Images

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amezuru Oman wakati maafisa wa Ukraine wakisema vikosi vyake vinawafurusha wanajeshi wa Urusi nje ya vijiji vilivyoko karibu na mji wa Kharkiv. 

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergey Lavrov amefanya ziara hiyo ya kushtukiza nchini Oman na kukutana na Sultan Haitham bin Tariq Al Said na kumuarifu kwa kifupi kuhusiana na vita hivyo, hii ikiwa ni kulingana na shirika la habari la serikali ya Oman.

Sultan Haitham ametilia msisitizo suala la kuheshimu misingi ya sheria ya kimataifa na kuimarishwa kwa juhudi za kidiplomasia za kusuluhisha mzozo huo, katika namna ambayo itaheshimu uhuru na uwepo wa mataifa hayo mawili pamoja na watu wake.

Vatikan Papst Franziskus im Rollstuhl
Papa Francis anatoa mwito wa kujizuia na vurugu na kusaka amani.Picha: Alessia Giuliani/Catholic Press Photo/ipa-agenc/picture alliance

Huko Vatican City, wake za wapiganaji wawili wa Ukraine waliokwama katika kiwanda cha chuma cha Azovstal katika mji wa Mariupol wamemuomba kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis kuwasaidia katika juhudi za kuwaokoa.

Kateryna Prokopenko na Yuliya Fedosiuk walizungumza na Papa Francis kwa dakika tano baada ya kumaliza ibada katika bustani ya Mtakatifu Petro mapema leo na kutoa ombi hilo, huku wakimuomba pia azungumze moja kwa moja na rais Vladimir Putin wa Urusi kuwaachia wapiganaji hao.

Papa Francis aliwaeleza wanawake hao kwamba ataendelea kuwaombea na kutoa mwito huu.

"Ninajiunga na viongozi wa kidini kuzihimiza pande zote kudumisha mtazamo wa amani na kujizuia na vurugu. Ninatoa wito kwa wahusika wote, kusikiliza matakwa ya watu na kuhakikisha haki za binadamu na uhuru wa raia unaheshimiwa kikamilifu." alisema Papa Francis.

Nchini Ukraine, rais Volodymyr Zelensky amesema vita vinavyoendelea nchini mwake vingeweza kuzuilika iwapo Kyiv ingekuwa mwanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO. Amenukuliwa akisema kama Ukraine ingekuwa mwanachama wa NATO kabla ya vita, labda hii leo kusingekuwa na vita.

Ukraine | Präsident Selenskyj
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky anasema kusingekuwa na vita kama wangekuwa wanachama wa NATOPicha: Präsidentschaft der Ukraine/ZUMA/dpa/picture alliance

Amesema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa chuo kikuu cha Sayansi cha Ufaransa kwa njia ya video na kuongeza kuwa alitaka kulilinda eneo la Ukraine hapo kabla na kumaliza mvutano na Urusi, na kuongeza kuwa bado milango ya majadiliano iko wazi. 

Mjini Moscow, mamlaka zilizowekwa na rais Putin katika mji wa Kherson, kusini mwa Ukraine imesema leo kwamba zinajipanga kuwasilisha ombi kwa kiongozi huyo wa Urusi kulichukua eneo hilo na kuwa sehemu ya Urusi. Kulingana na mamlaka hizo, wanataraji hadi mwezi Disemba eneo hilo litakuwa chini ya udhibiti kamili wa Urusi.

Kherson, eneo lililoko kaskazini mwa rasi ya Crimea iliyonyakuliwa na Moscow tangu mwaka 2014, lilikuwa jiji la kwanza kuangukia mikononi mwa Urusi baada ya uvamizi wa kijeshi nchini Ukraine, Februari 24 na lina umuhimu mkubwa kwenye rasi hiyo kwa kuisambazia maji ya kunywa na kumwagilia.

Mashirika: RTRE/AFPE/DW