1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lavrov na Kerry wakutana kuhusu Syria

12 Septemba 2013

Kabla ya mazungumzo ya Geneva rais Assad athibitisha utawala wake uko tayari kuziweka silaha zake za sumu chini ya uangalizi wa kimataifa kwa mujibu wa pendekezo la Urusi na sio kwa vitisho vya Marekani

https://p.dw.com/p/19gjp
Mawaziri wa nje wa Urusi na Marekani Sergei Lavrov na John Kerry
Mawaziri wa nje wa Urusi na Marekani Sergei Lavrov na John KerryPicha: AFP/Getty Images

Assad ametowa kauli hiyo katika mahojiano na televisheni ya Urusi akisema hatua hiyo haikuchukuliwa kutokana na vitisho vya Marekani bali ni kutokana na pendekezo la Urusi.Matamshi ya Assad yanakuja katika wakati ambapo mawaziri wa nje wa Marekani na Urusi wanakutana mjini Geneva kulijadili kwa kina pendekezo la Urusi katika mgogoro huo wa Syria.

Rais wa Syria Bashar Al Assad
Rais wa Syria Bashar Al AssadPicha: imago/UPI Photo

Rais Bashar al Assad ameliambia shirika la habari la Rossiya la Urusi kwamba silaha zake za sumu zitawekwa chini ya uangalizi wa Kimataifa kwasababu ya pendekezo la Urusi ni sio kufuatia kitisho cha Marekani.Waziri wa nje wa Marekani John Kerry anakutana na Sergei Lavrov ili kupata maelezo zaidi kuhusu mpango huo wa Urusi wa kuhusu silaha za sumu za Syria,mpango ambao unaweza kuepusha nchi hiyo ya Syria kuingiliwa kijeshi na Marekani.

Nia ya Marekani

Katika mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Marekani anatazamiwa kusisitiza kwamba mpango wowote utakaopitishwa unabidi kuilazimisha Syria kuchukuwa hatua za haraka kuonyesha inaweza kuaminiwa kuhusu kuachana na silaha zake za sumu.Awali Sergei Lavrov akizungumzia juu ya mkutano huo wa Geneva aliweka wazi nini kitakachojadiliwa kwa kina na kuepusha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Syria.

"Tumekubaliana kwamba tukiwa Geneva kwanza kujadiliana juhudi ambazo zimeungwa mkono kwa kiasi kikubwa duniani.juhudi ambazo ni kukubaliana kuziweka zana za sumu za Syria chini ya uangalizi wa kimataifa,sote tukielewa kwamba hatua hii itatowa nafasi ya nchi hiyo kutovamiwa kijeshi.

Hata hivyo kwa mujibu wa afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe,lengo la Marekani kufika katika mkutano huu wa Geneva ni kuona ikiwa kuna ukweli wowote katika pendekezo hilo la Urusi.Kerry pamoja na ujumbe wake wa wataalamu wanatarajia kukaa kwa muda wa alau siku mbili na wenzao warusi kujadiliana kuhusu suala hilo.

Shakashaka zipo

Waziri mkuu wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan
Waziri mkuu wa Uturuki Reccep Tayyip ErdoganPicha: Attila Kisbenedek/AFP/Getty Images

Tayari lakini kuna wanaoutilia shaka mpango huo, waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema utawala wa Assad huko nyuma umevunja ahadi zote na kuchukuwa nafasi hiyo kufanya mauaji ya halaiki.Erdogan ametanabahisha kwamba utawala wa Syria hauwezi kuaminiwa na kwamba unatafuta sababu ya kujiongezea muda.Halikadhalika kiongozi huyo wa Uturuki amesema mipaka ya Uturuki iko wazi kwa ajili ya wakimbizi kutoka Syria.Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza William Hague naye amesema nchi yake itaendelea kuwaunga mkono waasi nchini Syria.

Wakati wajumbe wakikusanyika mjini Geneva kuijadili Syria ndani ya taifa hilo vita vinaendelea,wanaharakati wanasema ndege za kivita zimeshambulia mojawapo ya hospitali kubwa iliyoko katika eneo linaloshikiliwa na waasi kaskazini mwa nchi hiyo,na kuuwa kiasi watu 11 ikiwemo madaktari wawili.Mkuu wa misaada wa Umoja wa Ulaya Kristalina Georgieva amesema vikosi vya serikali vimefanya uhalifu wa kivita kwa kuizuwia misaada ya vifaa vya matibabu na madawa vilivyokuwa vikisafirishwa katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi.

Mwandishi Saumu Mwasimba

Mhariri Mohammed AbdulRahman