1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lebanon yatimiza miaka 76 ya uhuru

Lilian Mtono
22 Novemba 2019

Lebanon inaadhimisha miaka 76 ya uhuru wake huku raia wake wakisema huu ndio mwaka pekee ambao wanahisi kuwa na uhuru wa kweli.

https://p.dw.com/p/3TYYP
Libanon 76. Unabhängigkeitstag
Picha: Reuters/M. Azakir

Wanasiasa hao wameonekana kwa pamoja kwenye gwaride hilo kwa mara ya kwanza tangu kulipoanza maandamano makubwa ya kitaifa yaliyosababisha serikali ya waziri mkuu Saad al-Hariri kujiuzulu.

Rais wa Lebanon Michel Aounspika wa bunge na waziri mkuu huyo aliyejiuzulu walikaa pamoja chini ya hema ya wizara ya ulinzi. Gwaride ambalo hufanyika katikati ya mji wa Beirut hii leo halikufanyika kwa kuwa bado eneo hilo linakaliwa na waandamanaji, ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu yalipoanza.

Rais Aoun alipotoa hotuba kwenye maadhimisho hayo ya uhuru amesisitiza kwamba huu sio muda wa kuzungumza na badala yake ni muda wa kufanya kazi. Amesema migongano ya kisiasa imeendelea kusababisha kucheleweshwa kuundwa kwa serikali mpya na kuongeza kwamba kunahitajia uangalifu mkubwa ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.

"Ndugu zangu waLebanon, ninawahutubia huku nikitambua kwamba huu sio wakati wa hotuba na sherehe. Ni wakati wa kufanya kazi kwa bidii kwa sababu tunakimbizana na wakati. Serikali mpya iliyosubiriwa na Lebanon ilitakiwa kuwa imeanza kazi. Lakini, mizozo inayodhibiti siasa za Lebanon imetulazimisha kuwa waangalifu ili kujiepusha na hatari zaidi, na kupata serikali itakayokidhi matarajio ya wengi." alisema Aoun kwenye hotuba aliyoitoa kupitia televisheni.

Libanon Proteste Sitzblockade
Waandamanaji wameendelea kusalia kwenye baadhi ya maeneo hata wakati wa maadhimisho hayo.Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Hussein

Taifa hilo limekumbwa na maandamano makubwa tangu Oktoba 17 yanayoshinikiza mabadiliko makubwa ya serikali. Maandamano hayo yaliwakusanya pamoja watu kutoka madhehebu mbalimbali huku wakiwa na matumaini kwamba shinikizo hilo litauondoa mfumo ambao wanadai umeshindwa.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa madhehebu tofauti nchini humo kuungana pamoja bila ya mwito kutoka chama cha siasa na kuvipinga vyama vyote, alisema mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu na kuongeza kuwa huo ndio uhuru na ulio dhahiri.

Novemba 23 mwaka 1943 Lebanon ilipata uhuru wake baada ya miaka 23 ya utawala wa Ufaransa, kutokana na wimbi la maandamano yaliyowaleta pamoja Wakristo na Waislamu. Hata hivyo taifa hilo lilijikuta katika wakati mgumu lilipoingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kati ya mwaka 1975 hadi 1990.

03.11.2019 Matangazo ya jioni

Rais Aoun bado amerejelea mwito wake kwa raia wa kufanyika mazungumzo, akisema hiyo ndio njia pekee ya kuusuluhisha mzozo huo.