Leipzig yaendelea kuongoza Bundesliga | IDHAA YA KISWAHILI | DW | 05.12.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

IDHAA YA KISWAHILI

Leipzig yaendelea kuongoza Bundesliga

Mechi nyingine katika wiki ya 13 ya msimu wa 54 wa ligi ya kandanda ya Ujeruamani, na ushindi mwingine kwa RB Leipzig. Timu hiyo ya Ujerumani Mashariki, imeshinda mechi nane mfululizo na kubaki kileleni mwa ligi.

Fußball Bundesliga FC Schalke 04 - RB Leipzig

Timo Werner wa Leipzig akianguka eneo la hatari bila kuguswa na kipa wa Schalke, Ralf Fährmann

Leipzig walikuwa katika nafasi ya pili kabla kucheza na Schalke na kuishinda kwa mabao 2-1. Ushindi wa Leipzig umeibua mjadala mkubwa kufuatia hatua ya mwamuzi Bastian Dankert kutoa mkwaju wa penalti baada ya mshambuliaji wa Leipzig Timo Werner kujiangusha katika eneo la hatari la lango la Schalke, sekunde 19 baada ya mechi kuanza. Werner aliipa timu yake bao la kwanza kupitia mkwaju huo wa penalti lakini baadaye mchezji wa Schalke Saed Kolasinac akasawazisha kabla kipindi cha mapumziko. Katika kipindi cha pili Saed Kolasinac alijifunga mwenyewe na kuwapa Leipzig goli la pili.

Nahodha wa Schalke Benedikt Höwedes alisema, "Tumechangia wenyewe kwa kiwango kidogo matokeo haya, kwa sababu hatukucheza vizuri katika kipindi cha pili. Leipzig walikuwa wazuri sana na wameshinda mfululizo kwa haki kabisa. Lakini ikiwa tofauti ya magoli ndiyo inayoamua mshindi, kupitia mchezaji kujiangusha wazi aktika eneo la hatari na kupewa penalti, basi ni jambo linalotia uchungu."

Leipzig inaongoza ligi na pointi 31 ikifuatiwa na Bayern Munich katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 30 baada ya kuishinda Mainzi 3-1 siku ya Ijumaa.

Weder Bremen yapata pigo

Weder Bremen ilipata pigo jana wakati kiungo wake Izet Hajrovic alipopata jeraha baya la goto ambalo huenda likamfanya asicheze tena msimu huu. Hajrovic alitolewa nje kwenye machela wakati wa mchuano kati ya Bremen na Ingolstadt ambapo Bremen ilishinda kwa mabao 2-1. Fin Bartels aliisaidia timu yake kutoroka na pointi tatu. "Bila kujali tumecheza vipi leo na kurudia makos agani, ilikuwa muhimu mno kupata pointi tatu. Michezo ya namna hii pengine inatupa hali ya kujiamini zaidi. Tena mtu unatulia zaidi kucheza mechi hizi hadi mwisho. Hilo ndilo linalotakiwa kuwa lengo na tunatakiwa kuendelea kulifanyia kazi," alisema Bartels.

Fußball Bundesliga Hoffenheim vs. 1. FC Köln

Sandro Wagner wa Hoffenheim akifunga bao la tatu la timu yake

FC Cologne ilipoteza mechi yake ya pili msimu huu kwa kukandikwa magolo manne kwa bila na Hoffenheim, mechi iliyochezwa katika uwanja wa Wirsol Rhein Neckar Arena mjini Hoffenheim. Sandro Wagner aliipatia Hoffenheim bao la kwanza dakika ya nane ya mchezo. Jeremy Toljan alifunga la pili kabla Wagner kuongeza la tatu. Na hatimaye Mark Uth aliyezaliwa katika mji wa Cologne akagonga msumari wa mwisho katika jeneza la Cologne.

Kuhusu matokeo hayo kocha wa FC Cologne, Peter Stöger, alisema, "Katika soka tunatakiwa kutumia fursa zote. Wachezaji wa Hoffenheim wamefanya hivyo vizuri sana, lakini sisi licha ya kupata nafasi nzuri tatu, nne za kufunga, hatukuzitumia. Na ndio maana matokeo yakawa hivi. Lakini kimsingi matokeo haya hayatoi maamuzi ya mwisho, kama tungetoka bao moja kwa bila na kujadili vipi tulivyokaribia kushinda. Mambo yamekwenda mrama kweli kweli. Wapinzani wetu Hoffenhemi wametumia fursa nyingi. Si sadfa pia kwamba hawajapoteza mechi yoyote msimu huu.

Mwandishi: Josephat Charo

Mhariri: Saumu Yusuf