1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Leo ni siku ya watoto wa mitaani duniani

George Njogopa12 Aprili 2018

Tatizo la watoto wa mitaani limezidi kuwa kubwa ambapo watoto wa mitaani wanalazimika kufanya kazi ngumu ili kujikimu kimaisha

https://p.dw.com/p/2vwfE
Straßenkinder in Kampala Uganda
Picha: DW/F. Yiga

Leo ni siku ya watoto wa mitaani duniani na huko nchini Tanzania tatizo hilo limeendelea kuwa kubwa huku baadhi ya watoto wakilazimika kufanya kazi ngumu za mitaani kama vile kuosha magari na hata kuokoteza vyuma ili waweze kujikimu kimaisha.

Serikali imekiri hivi karibuni kuwepo kwa ongezeko la watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani hasa katika miji mikubwa nchini ambapo takwimu zinaonesha kuwa Jiji la Dar es salaam linaongoza kwa asilimia 28 ya watoto hao ikifuatiwa na miji mingine kama Mwanza, Dodoma na Tanga.

Hata hivyo, imesema inachukua hatua za kukabiliana na hali hiyo kwa kuboresha huduma za kijamii. Huku wakiwa katika mazingira hatarishi wengi wa watoto hao wanajitumbukiza kwenye makundi kama vile utumiaji wa sigara, udokozi na hata uporaji mdogo mdogo kwa minajiri ya kupata chochote kwa ajili ya kusukuma maisha yao, kama alivyosimulia mmoja wao.

Watoto wanaorandaranda hujikimu kwa shida

Watoto wa mitaani mjini Dar es Salaam wakiomba msaada kutoka kwa watu
Watoto wa mitaani mjini Dar es Salaam wakiomba msaada kutoka kwa watuPicha: Ericky Boniphace

Ingawa kwa ujumla wanaishi kwa shida baadhi ya watoto wanalazimika kujitumbukiza katika ajira zisizo rasmi kama vile uuzaji wa vitu kama karanga, mihogo huku wengine wakizunguka katika maeneo yenye msongamano wa magari wakiyawinda magari yanayosimama na kuyaonya kwa mategemeo ya kupata ujira wa angalu mia moja mpaka mia mbili.

Mtoto huyu anasema ameamua kufanya kazi ya kuonya magari kwa vile hapendi kuona akitumbukia kwenye matatizo.

Kuna mambo mengi yanayowafanya watoto kutumbukia kwenye madhila hayo ikiwamo yale yanayosababishwa na wazazi na wakati mwingine watoto wenyewe kuwa na shauku ya kujaribu maisha mapya katika maeneo ya mijini.

Utamaduni wa jamii ni suluhisho kwa tatizo hili?

Hata hivyo jamii ya wamasaai ni moja ya makabila machache ambayo ni nadra kuona watoto wao wakirandaranda mitaani.

Mama mmoja wa kimasaai amesema, hilo linawezekana kwa vile watoto hao wanalelewa kwa kufuata misingi inayoakiasi mila na utamaduni wa jamii yao.

Wachambuzi wa mambo wanasema tatizo la watoto wa mitaani ni sawa na bomu liliachwa bila kuteguliwa na wakati wowote linaweza kulipuka na kuzidisha hali mbaya katika ustawi wa kijamii.

Kelvini Mata anasema kuibuka kwa makundi ya kihalifu kama yale yafahamikayo Panyaroad ni moja ya matokeo ya kuongezeka kwa watoto wa mitaani.

Takwimu zinazoonyesha kuwa watoto milioni 2.5 wamekuwa yatima baada ya wazazi wao kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Mwandishi: George Njogopa

Mhariri: Iddi Ssessanga