1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Liberia yatangaza amri ya kutotoka nje usiku

Josephat Nyiro Charo20 Agosti 2014

Tangazo hilo la Jumanne (19.08.2014) ni jitihada za kukabiliana na ugonjwa hatari wa Ebola. Umoja wa Mataifa unamtuma mjumbe wake Afrika Magharibi kusaidia utoaji wa huduma za afya.

https://p.dw.com/p/1CxLK
Ebola / Liberia / Monrovia
Picha: Reuters

Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf ametangaza amri ya kutotoka nje usiku na kuviweka karantini vitongoji viwili, kimoja cha mji mkuu Monrovia cha West Point, katika juhudi za kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa Ebola. Amri hiyo itaanza kutekelezwa leo saa tatu usiku hadi saa kumi na mbili asubuhi. Rais Sirleaf amesema maeneo yote ya burudani yatafungwa na vituo vyote vya video vitatakiwa kufungwa saa kumi na mbili jioni.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, linaongeza juhudi za kupeleka msaada wa dharura wa chakula kwa maeneo yaliyowekwa katika karantini, yanayojumuisha maeneo yaliyoathirika sana kama vile Bomi na Foya nchini Liberia.

Afisa wa kitaifa wa uratibu wa shirika hilo, Etienne Christopher Saint Jean alisema, "Operesheni imekuwa kubwa na tunapanga kuitanua kukiwa na haja ya kufanya hivyo. Ukienda nchi nyingine utakuta operesheni kama hii ikiendelea na tunataka kuchukua hatua za tahadhari badala ya kusubiri tatizo litokee ndio tuchukue hatua."

Sierra Leone yatangaza maambukizi mapya

Wakati haya yakiarifiwa Sierra Leone imeripoti visa takriban 200 vya maambukizi mapya ya Ebola. Mjumbe wa shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, Glen Myers, amesema watu hao walioambukizwa wamewekwa karantini, wengi wao wakiwa katika hali ya kutia wasiwasi. Myers aidha amesema visa hivyo maambukizi vilikuwa tayari vimeripotiwa wiki hii katika mji wa Lunar katika wilaya ya Port Loko.

Ebola West Point Slum Infizierte verlassen Isolierstation
Wagonjwa wa Ebola, katika kitongoji cha West PointPicha: John Moore/Getty Images

Wizara ya afya ya Sierra Leone imesema kijana aliyeambukizwa Ebola katika mji mkuu Freetown, alikimbia kutoka hospitali ya Connaught,ambako alikuwa akitibiwa. Kijana alipatikana saa chache baadaye katika nyumba ya wazazi wake na kulazwa tena katika kituo maalumu kinachowashughulikia wagonjwa wa Ebola. Wizara hiyo imesema inawatafuta watu wote waliokutana na kijanahuyo.

Nchini Nigeria, daktari bingwa aliyemtibu mgonjwa wa kwanza wa Ebola katika taifa hilo amekufa hivyo kuongeza idadi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa huo nchini humo kufikia watano.

Umoja wa Mataifa wamtuma mjumbe maalumu wa Ebola

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa unamtuma mjumbe mpya atakayeshughulikia Ebola, mtaalamu wa afya ya jamii na daktari wa Uingereza, David Nabarro, kwenda Afrika Magharibi kusaidia kupambana na ugonjwa wa Ebola katika nchi nne zilizoathiriwa na janga hilo. Akizungumza mjini New York Nabbaro alisema, "Nitaanzisha mpango madhubuti Afrika Magharibi pamoja na wenzetu wanaofanya kazi na serikali na wadau wengine kutathimini njia nzuri ambazo mfumo wetu mzima wa Umoja wa Mataifa unaweza kuwasaidia watu, jamii na serikali zilizoathiriwa na ugonjwa wa Ebola."

Vogelgrippe Konferenz in Peking China David Nabarro
Mjumbe maalumu kuhusu Ebola, David NabarroPicha: AP

Nabarro atafanya mikutano leo na maafisa wa Benki ya Dunia na Taasisi za kudhibiti na kuzuia magonjwa za Marekani mjini Washington na baadaye jioni atasafiri kwenda Dakar, Senegal kabla kuelekea Monrovia, Freetown, Conakry na Abuja. Katika safari yake ataandamana na Keiji Fukuda, naibu mkurugenzi mtendaji wa masuala ya afya wa shirika la afya duniani, WHO.

Nabarro amewaambia waandishi wa habari mjini New York atafanya mazungumzo na tume ya Umoja wa Mataifa nchini Liberia kuhusu njia ambazo wanajeshi wa kulinda amani wa tume hiyo wanaweza kusaidia kukabiliana na athari za ugonjwa huo.

Benki ya Maendeleo ya Afrika yatoa msaada

Kwa upande mwingine, benki ya maendeleo ya Afrika imeahidi kutoa dola milioni 60 kusaidia mapambano dhidi ya Ebola. Rais wa benki hiyo, Donald Kaberuka, amesema msaada huo utazisadia serikali za Guinea, Liberia, Sierra Leone na Nigeria kuimarisha ufuatiliaji na mifumo ya kuchukua hatua kukomesha kuenea ugonjwa huo hatari.

"Janga la Ebola sio tatizo la kiafya tu bali pia ni janga la kiuchumi linaloziathri sekta nyingi," akasema Kaberuka wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Abidjan, Cote d'Ivoire.

Janga la Ebola Afrika Magharibi ndilo baya zaidi tangu kirusi kinachosababisha ugonjwa huo kilipogunduliwa kwa mara ya kwanza miingo minne iliyopita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Shirika la Afya duniani, WHO, limesema siku ya Jumanne kirusi cha Ebola kimewaua watu 84 katika kipindi cha siku tatu, na hivyo kuifanya idadi ya vifo kutokana na ugonjwa huo kufikia 1,229. Watu wapatao 2,240 wamethibitishwa au wameshukiwa kuuguwa ugonjwa huo.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/DPAE

Mhariri: Daniel Gakuba