1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yatakiwa kurekebisha sheria ya kinga kwa wanamgambo

11 Mei 2012

Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limeitaka Libya kurekebisha haraka sheria zake zinazowapa kinga wanamgambo walioumuondoa Muammar Gaddafi ambao wamefanya vitendo vya uhalifu wa kivita.

https://p.dw.com/p/14teJ
Serikali ya Baraza la Kitaifa la Libya
Serikali ya Baraza la Kitaifa la LibyaPicha: REUTERS

Naibu Mkurugenzi wa Human Rights Watch kwa Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini, Joe Stork, amesema kwamba Baraza la Mpito la Libya linapaswa kuifanyia marekebisho sheria hiyo mpya, ambayo inawalinda na mashitaka watu waliofanya uhalifu, ikiwa "matendo yao yalidhamiria kuinua na kulinda mapinduzi" yaliyomng'oa madarakani Gaddafi.

Stork amesema sheria hiyo inawaruhusu watu waliofanya uhalifu mkubwa kutembea wakiwa huru kwa kisingizio cha siasa, jambo ambalo linakinzana na mapambano dhidi ya utamaduni wa kulindana, ambao Walibya walipigania kuuondosha.

Sheria 38, kama inavyojulikana sheria hiyo mpya inayoanza kutumika rasmi hapo kesho, inaeleza kwamba hakutakuwa na mashitaka wala adhabu kwa matendo ya kijeshi, kiusalama au kiraia ambayo yalifanywa na wanamapinduzi kwa dhamira ya kuhakikisha mafanikio ya mapinduzi hayo.

Sheria hiyo pia inaipa serikali madaraka ya kudhibiti matendo ya mtu, kumpiga faini, au kumuweka kizuizini hadi miezi miwili ikiwa mtu huyo anachukuliwa kuwa ni hatari kwa usalama wa taifa, kwa mujibu wa cheo chake kwenye utawala uliopinduliwa.

Makundi ya haki za binaadamu yanasema kwamba uhalifu wa kivita ulifanywa na pande zote mbili wakati wa mgogoro wa mwaka jana. Makundi hayo yameonya dhidi ya kuendelea kwa mateso katika kambi zinazodhibitiwa na wanamgambo.

Sheria hiyo mpya inawaamuru mawaziri wa ulinzi na mambo ya ndani kuwafikisha mahakamani wapiganaji waliokamatwa na waasi wa zamani au kuwaachia huru ifikapo tarehe 12 Julai, ikiwa hakuna ushahidi wa kutosha dhidi yao. Stork ameikaribisha hatua hiyo aliyoiita ni nzuri kwa sasa.

Sheria nyengine zilizopitishwa mwezi huu, kama ile inayofanya iwe ni uhalifu kuutukuza utawala wa Gaddafi, zimezua utata na kupingwa vikali na makundi ya haki za binaadamu.

Umoja wa Mataifa wasema maelfu washikiliwa na wanamgambo

Taarifa ya Human Rights Watch imetoka muda mfupi tu baada ya Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Libya, Ian Martin, kuliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kwamba maelfu ya watu wanaotuhumiwa kuwa wafuasi wa Gaddafi, bado wanashikiliwa katika mahabusu za siri za wanamgambo wa Libya.

Wanamgambo wa Libya katika eneo la Sabha.
Wanamgambo wa Libya katika eneo la Sabha.Picha: Reuters

Martin aliliambia Baraza hilo hapo jana, kwamba wengi kati ya mahabusu hao wanateswa. Alisema magereza mengi bado yanashikiliwa na wapiganaji waliosaidia kumuondoa Gaddafi madarakani, na aliyataja magereza hayo kuwa ni "kikwazo kwa utawala wa sheria".

Mjumbe huyo alionesha wasiwasi wake kuhusiana na sheria hizo zinazowapa kinga wapiganaji walioshiriki kuuangusha utawala wa Gaddafi, ingawa alisema Libya inapiga hatua nzuri kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia wa mwezi ujao.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/DPA
Mhariri: Daniel Gakuba