1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yazama katika bahari ya damu

13 Novemba 2014

Mabomu yameripuliwa karibu na ofisi za ubalozi wa Misri na falme za nchi za kiarabu-Emireti katika mji mkuu wa Libya-Tripoli. Majumba na maduka ya karibu na ofisi hizo yameharibiwa.

https://p.dw.com/p/1DmHT
Shambulio la bomu Karibu na ubalozi wa Misri mjini TripoliPicha: M. Turkia/AFP/Getty Images

Miripuko hiyo ya mabomu yamefuatia mlolongo wa mashambulio ya mabomu yaliyotegwa ndani ya magari yaliyotokea jana na hasa katika miji inayodhibitiwa na serikali inayotambuliwa na jumuia ya kimataifa yenye makao yake mjini Tobrouk,mashariki ya Libya-serikali ambayo uhalali wake unabishwa na serikali hasimu ya mjini Tripoli.

Ripota wa shirika la habari la Reuters amesema bomu lililoripuliwa karibu na ofisi ya ubalozi wa Misri limebomoa majumba kadhaa na maduka,lakini hakuna hasara ya maisha iliyopatikana kwakua ubalozi huo ulikuwa umefungwa.Madirisha ya vigae ya ubalozi huo yamevunjika na magari yaliyowekwa karibu na hapo yamehujumiwa.

Duru kutoka falme za nchi za kiarabu zinasema ofisi yao ya ubalozi mjini Tripoli nayo pia imeshambuliwa lakini ilikuwa pia tupu.Walinzi waliokuwa nje ya ofisi hiyo ya ubalozi wamejeruhiwa.

Misri na falme za nchi za kiarabu au Emirati ni miongoni mwa nchi zilizowahamisha watumishi wa ofisi zao za ubalozi kutoka Tripoli tangu yalipoanza mapigano ya makundi kadhaa ya wanamgambo wanaohasimiana kuania kuudhibiti mji mkuu wa Libya.

Miaka mitatu baada ya kung'olewa madarakani na kuuliwa Muammar Gaddafi,Libya ingali bado imezama katika bahari ya vurugu,makundi tofauti ya wanamgambo wakiwania madaraka na udhibiti wa visima vya mafuta.

Mojawapo ya makundi hayo,linalotokea Misrata,limeuteka mji mkuu Tripoli msimu wa kiangazi uliopita na kuunda serikali na bunge,na kuwalazimisha wakati huo huo wabunge waliochaguliwa na wananchi na serikali ya waziri mkuu Abdallah al Thinni kukimbilia Tobrouk.

Mahasimu wa Abdallah al Thinni wanaituhumu Misri kumuunga mkono jenerali wa zamani,Khalifa Haftar ,anaeongoza opereshini ya kuwatimua wanamgambo wa kiislam toka mji wa mashariki wa Benghazi.

Na juhudi za upatanishi zinazoendeshwa na Umoja wa mataifa hadi wakati huu hazikuleta tija.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu