1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Libya yazidi kuwaka moto huku Muammar Gaddafi akiendelea kukwamia madaraka

3 Juni 2011

Mashambulizi ya angani ya jumuiya ya kujihami ya NATO yanaendelea katika mji mkuu wa Libya Tripoli, huku Ufaransa na China zikiendeleza juhudi za kujaribu kuutatua mzozo huo

https://p.dw.com/p/11TWz
Moshi wafuka juu ya jengo mjini Tripoli baada ya shambulizi la angani la NATOPicha: picture alliance/dpa

Ufaransa imesema leo kuwa inashirikiana na marafikii wa karibu wa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi ili kujaribu kumshawishi aondoke madarakani, pamoja na kuongeza shinikizo la kijeshi wakati huu ambapo awamu ya pili ya operesheni ya miezi minne ya jumuiya ya kujihami ya NATO imeanza nchini Libya.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Alain Juppe amekiambia kituo cha redio Europe 1 kuwa, Gaddafi sasa anaedelea kutengwa, kwa sababu maafisa wakuu wameendelea kujitenga na serikali yake, na kwamba wamepokea ripoti kutoka kwa wandani wake wa karibu wanaoelewa kuwa ni sharti aondoke. Amesema wataendeleza shinikizo la kijeshi jinsi walivyofanya katika siku za hivi karibuni, lakini wakati huo huo wanazungumza na kila mtu aliye na uhusiano wa karibu naye ili wamshawishi aondoke madarakni.

NATO-Generalsekretär Rasmussen
Katibu Mkuu wa jumuiya ya NATO Anders Fogh Rasmussen akizungumza na wandishi habariPicha: AP

Jumuiya ya kujihami ya NATO iliongeza muda wa operesheni zake za kuwalinda raia nchini Libya kwa siku nyengine 90 wiki hii, baada ya Gaddafi kuonyesha wazi kuwa hataondoka madarakani hata wakati mapigano yaliyodumu kwa miezi minne sasa yakiendelea nchini mwake na kusababisha vifo vya maelfu ya watu.

Waasi wa Libya na jumuiya ya NATO wanasema kuondoka kwa Gaddafi ndiko kunaweza tu kuwafanya wakubali kuweka chini silaha, lakini naye alimwambia wazi rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma aliyemtembelea wiki hii kuwa hataondoka Libya.

Mkuu wa shirika la kitaifa la mafuta ambaye pia alikuwa waziri wa mafuta wa Libya Shokri Ghanem alikuwa kiongozi wa hivi punde tujitenga na serikali ya Gaddafi siku ya jumatano, siku mbili tu baada ya kujiuzulu kwa maafisa wanane wakuu wa jeshi wakiwemo majenerali watano, na wale wa wiki za hapo kabla, mabalozi wakuu na mawaziri wa zamani.

Wakati huo huo balozi mmoja wa China amekutana na kiongozi wa waasi wa baraza la kitaifa la mpito ambalo linapigana kumtimua uongozini Gaddafi. Taarifa kutoka kwa msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Hong Lei haikufichua maelezo ya mkutano huo baina ya balozi wa China nchini Qatar Zhang Ziliang, na Mustafa Abdel Jalil, ambaye ni mwenyekiti wa baraza hilo.

Nako nchini Marekani, spika wa baraza la wawakilishi John Boehner atawasilisha azimio hii leo linalomtaka rais Barrack Obama aeleze kuhusu uamuzi wake wa kushiriki operesheni za mashambulizi nchini Libya, wakati bunge likitilia shaka operesheni hizo. Obama atahitajika kulieleza bunge ni kwa nini hakutafuta idhini ya kuvikubalia vikosi vya Marekani kuungana na operesheni hiyo inayoongozwa na jumuiya ya NATO.

Na hayo yakijiri, Miripuko kadhaa imesikika jana usiku na mapema leo katika mji mkuu wa libya Tripoli, ambao umelengwa na mashambulizi ya angani ya jumuiya ya kujihami ya NATO kwa siku kadhaa sasa.

Miripuko minne kwanza ilisikika saa tano usiku hapo jana katikati mwa mji wa Tripoli, na kufwatwa na mingine dakika 15 baadaye. Kisha usiku wa manane kukawa na miripuko mingine minne mizito iliyotikisa wilaya ambayo makao ya Gaddafi yanapatikana sio mbali sana kutoka katikati ya mji. Kambi za kijeshi katika eneo hilo pia zililengwa katika mashambulizi kadhaa wiki iliyopita. Mapema wiki hii msemaji wa serikali Mussa Ibrahim alisema mashambulizi ya angani ya NATO dhidi ya Libya yamewauwa raia 718 na kuwajeruhi 4,067 tangu yalipoanzishwa tarehe 19 mwezi machi hadi Mei 26.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Abdul-Rahman