1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya mabingwa barani Ulaya, Mourinho ajiwinda kumsukuma Sir Furgeson

Aboubakary Jumaa Liongo/AFP10 Machi 2009

Patashika hiyo ya ligi ya mabingwa barani Ulaya leo hii itashuhudia mechi nne, lakini macho na masikio yataelekezwa zaidi huko Old Trafford kati ya wenyeji na mabingwa w atetezi Manchester United na Inter Milan.

https://p.dw.com/p/H9Gh

Katika mechi ya kwanza iliyofanyika Milan timu hizo ziliumaliza mpambano bila ya mtu kuufumania mlango wa mwenziye.


Matokeo hayo yameiweka Man United katika nafasi nzuri ya kuisukuma nje Inter ambayo inafundishwa na kocha wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho

Ijapokuwa wengi wanaamini kuwa Manchester United wataibuka na ushindi hii leo, lakini Mourinho ni mtu ambaye anajulikana kwa kuweza kubadilisha hali ya mchezo na kugeuza matokeo.


Washabiki wa Manchester United bado wanayo kumbukumbu ya miaka mitano iliyopita wakati huo Mourihno akiwa kocha wa FC Porto ya Ureno alipojumuika na wachezaji wake kushangilia ushindi wa jumla ya mabao 3-2 na kuiondosha mashindanoni MANU.


Ni mtu anayejua kuweka mikakati na kutambua werevu wa timu pinzani pale wanaporudiana.Mfano ni wiki mbili zilizopita katika mechi ya kwanza huko San Siro ambapo vijana wa Sir Alex Ferguson waliweza kudhibiti mchezo katika kipindi cha kwanza na kukosa nafasi karibu tatu au nne za kupachika mabao.


Lakini katika kipindi cha pili Mourinho alifanya mabadiliko kwa kumtoa beki wa kati Nelson Rivas na kumuingiza mkongwe Ivan Cordoba kuimarisha ulinzi nyuma na hivyo kumpa nafasi kiungo Estaban Cambiasso kupeleka mashambulizi zaidi mbele kuliko kulinda lango.


Pia akamuelekeza kiungo mwengine Javier Zanetti kucheza zaidi wingi ya kulia na kumzuia beki wa Manchester United anayepanda mara kwa mara Evra kufanya hivyo.


Kocha wa Manchester United Sir Alex Ferguson anahisi kuwa Mourinho atatumia mbinu za kujihami zaidi hii leo ili mpambano huo ufikie katika hatua ya kupigiana mikwaju ya penalti.


Lakini anasema hana wasi wasi na hilo, kwani vijana wake wameonesha wanaweza kufanya chochote kinachotakiwa kufanywa hata wakati wa penalti.

Makocha hao wamekuwa katika vita vya maneno kwa muda mrefu, na mwishoni mwa wiki Mourinhno alisema kuwa angependa kurithi mikoba ya mzee Ferguson pale atakapoamua kustaafu Old Trafford, ingawaje Sir Ferguson akiwa na umri wa miaka 67 hajaonesha ishara yoyote ya kuondoka.


Timu hizo zimewahi kukutana mara tatu ambapo kila moja imeshinda mara moja na kutoka sare moja


Mechi nyingine leo hii, zitakuwa ni kati ya Atletico Madrid itakayokuwa ugenini kucheza na FC Porto, ambapo katika mechi ya kwanza timu hizi zilitoka sare ya mabao 2-2.


Timu nyingine ya Uhispania Barcelona ikiwa na faida ya goli la ugenini kufuatia sare ya bao 1-1 inaikaribisha Olympique Lyon ya Ufaransa timu ambayo huwa haitabiriki.


Nayo Arsenal itasafiri hadi Roma Italia kujaribu kulinda bao lake ililopata katika mechi ya kwanza wiki mbili zilizopita jijini London.