1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ligi ya Mabingwa Ulaya:Bremen na Schalke 04 zajiwinda kushinda

20 Oktoba 2010

Baada ya hapo jana Bayern Munich kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya CFR ya Romania, leo ni zamu ya Werder Bremen na Schalker 04 kuendelea wimbi la ushindi kwa timu za Ujerumani, pale zitakaposhuka dimbani.

https://p.dw.com/p/PjRo
Wachezaji wa Bremen wakishangilia ushindi dimbaniPicha: dapd

Bremen watakuwa ugenini kupambana na mabingwa wa Uholanzi FC Twente Enschede, Huku Schalker wakiwakaribisha Hapoel Tel Aviv ya Israel.

Werder Bremen inahitaji sana kushinda mpambano huo wa leo, ili kufufua matumaini ya kuweza kufuzu kwa duru ijayo ya mtoano, baada ya kuchapwa mabao 4-0 na mabingwa watetezi Inter Milan katika mechi iliyopita.

Mshambuliaji wa timu hiyo Claudio Pizarro amesema kuwa wanahitaji kwa udi na uvumba ushindi katika mechi hiyo.Bremen ilifungwa bao 1-0 na wadachi hao kwenye uwanja huo huo February mwaka huu katika michuano ya awali ya ligi ya Ulaya, kabla ya kujibu mapigo katika mechi ya marudiano kwa kuichapa mabao 4-1.

Eran Zahavi während des Trainings für das Spiel FC Schalke 04 vs. Hapoel Tel Aviv
Wachezaji wa Schalke wakijiwinda kwa mechi ya leoPicha: AP

Schalke kwa upande wao wanategemewa kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani, kushinda pambano hilo na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu, ambapo mpaka sasa wanakamata nafasi ya pili katika kundi B wakiwa na pointi 3 nyuma ya Olympic Lyon wenye pointi 6.

Mshambuliaji wa timu hiyo aliye katika kiwango cha juu hivi sasa Klaas-Jan Huntelaar anategemewa kuongoza mashambulizi ya Schalke akisaidiana na Raul.

Katika mechi nyingine hii leo, Samuel Et´oo ataongoza safu ya ushambuliaji ya mabingwa watetezi Inter Milan kuwakaribisha Tottenham Hotspur ya Uingereza, huku Manchester United ikiwa mwenyeji wa Bursaspor.

Kocha wa Manchester United Sir Alex anajaribu kuyaweka pembeni mawazo kufuatia kauli ya mshambuliaji tegemezi wa timu hiyo Wyne Rooney kutaka kuondoka, nakuelekeza fikra zake katika mechi hiyo.

Nayo Barcelona itakuwa nyumbani Nou Camp kuumana na FC Copenhagen, il hali Benfica ya Ureno ikiwa mgeni wa Olympic Lyon mjini Paris. 

Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameondoa tofauti zake na shirikisho la kabumbu la Ujerumani DFB kutokana na kitendo chake cha kwenda bila taarifa katika chumba cha kubadilishia nguo cha timu ya taifa ya Ujerumani mara baada ya timu hiyo kuifunga Uturuki mjini Berlin mabao 3-0.

Kansela Merkel anayefahamika kwa unazi wake mkubwa wa kabumbu akiongozana na Rais Christian Wulff na mtoto wake wa kike alikwenda bila shirika hilo kuwa na taarifa kuwasalimia wachezaji, kitendo kilichowakasirisha wakuu wa shirika hilo la DFB.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/DPA

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman